Watu 8 wauawa katika shambulio kusini mashariki mwa Iran
26 Julai 2025Vyombo vya habari vya serikali vimelitaja shambulio hilo kuwa "la kigaidi", na kuripoti kuwa watu wasiojulikana wenye silaha walishambulia leo asubuhi kituo cha mahakama mjini Zahedan, mji mkuu wa jimbo la Sistan-Baluchistan kusini-mashariki mwa Iran.
Shirika rasmi la habari la IRNA liliripoti kuwa washambuliaji watatu waliuawa wakati wa shambulio hilo. Kulingana na Alireza Daliri, naibu kamanda wa polisi wa jimbo la Sistan-Baluchistan, washambuliaji walijaribu kuingia katika jengo hilo wakijifanya kuwa wageni.
Daliri amesema washambuliaji walirusha bomu la mkono ndani ya jengo hilo, na kuua watu kadhaa waliokuwamo, wakiwemo mtoto mchanga wa mwaka mmoja na mama yake.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, kundi la kijihadi la Jaish al-Adl, ambalo lina makao yake nchini Pakistan lakini pia linafanya shughuli zake Iran, limedai kuhusika na shambulio hilo.