Watu saba wauawa kwenye maandamano ya Togo
1 Julai 2025Taarifa ya pamoja iliyotolewa na mashirika kumi na mbili ya haki za binadamu nchini humo, imevituhumu vyombo vya usalama kwa kufanya ukamataji kiholela, kuwapiga na kuwatesa raia pamoja na kuiba na kuharibu mali binafsi za raia.
Mashirika hayo yamesema katika miili mitatu, miwili ikiwa ya watoto wadogo ilipatikana siku ya Ijumaa katika eneo la Be Lagoon mashariki mwa mji mkuu, Lome.
Aidha mashirika hayo yaliongeza kuwa miili mingine ya ndugu wawili ilipatikana siku hiyo hiyo katika ziwa lililopo katika eneo la Akodessewa huku siku ya Jumamosi maiti mbili zilipatikana eneo la Nyekonakpoe.
Msemaji wa shirika la kiraia la FCTD, David Dosseh, amesema kinachoshuhudiwa kwa sasa nchini Togo ni umwagaji wa damu za raia wasio na hatia.
"Janga hili limegeuka kuwa la kikatili na kusikitisha zaidi baada ya taarifa za kupatikana kwa miili ya watu waliopoteza maisha, wakiwemo watoto wadogo." Alisema mbele ya waandishi wa habari.
Aliongeza kwamba "kwa mara nyingine tena, ardhi ya Togo imelowa damu za watu wasio na hatia- damu za watoto wetu- na sasa imetosha."
Kwa upande wa serikali ilikiri kupatikana kwa miili hiyo katika eneo la Be lagoon na ziwa Akodessewa lakini ikisema vifo hivyo vilisababishwa na kuzama majini.
Waandamanaji likiwemo wale wanaoendesha vugu vugu la "Don't Touch My Constitution” wakipinga mabadiliko ya katiba, linalojumuisha vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia, lilitoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu uhalifu uliofanyika katika siku tatu za kile walichokiita 'ukandamizaji'. wanasema hawatatoka mtaani hadi pale Rais Gnassingbe atakapoachia madaraka.
"Kile tunachokitaka kwa sasa ni Faure Gnassingbe kujiuzulu. Tutaendelea kuandamana hata baada ya siku tatu hadi hapo atakapoachia madaraka."
Mmoja wa waandamanaji alipaza sauti wakati vikosi vya usalama vikivurumisha gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.
Msingi wa maandamano ya Togo
Katika miaka ya hivi karibuni maandamano yamekuwa ni nadra nchini Togo, lakini maandamano ya karibuni ni ya pili kwa mwezi huu wa Juni.
Maandamano ya awamu hii yanalenga kupinga kukamatwa kwa wakosoaji wa serikali, kupanda kwa gharama ya maisha, na mabadiliko ya katiba yaliyoruhusu Faure Gnassingbe kuimarisha zaidi mamlaka yake.
Takribani watu 50 wamekamatwa na mamlaka kati ya Juni 5 na 6, huku polisi ikitumia nguvu katika kuwatawanya waandamanaji. Waziri wa Mageuzi ya Utumishi wa Umma, Kazi na Mazungumzo ya Kijamii nchini Togo, Gilbert Bawara, wiki iliyopita alisema kulikuwa na "nia dhahiri ya kuleta vurugu na machafuko”.
Vuguvugu la "Don't Touch My Constitution” limewataka wapinzani kususia uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Julai 17, na kuuita 'uchaguzi wa maigizo'.
Ikumbukwe, familia ya Gnassingbe inaiongoza Togo kwa takribani miongo sita huku Rais Faure akiongoza tangu 2005.