Watu milioni 83 wageuka wakimbizi wa ndani duniani
13 Mei 2025Ripoti ya pamoja ya mwaka huu iliyotolewa Jumanne na Kituo cha Kimataifa Kinachofuatilia Wakimbizi wa Ndani, IDMC, pamoja na Baraza la Wakimbizi la Norway, NRC, imeeleza kuwa idadi hiyoni zaidi ya mara mbili ya miaka sita iliyopita.
Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya wakimbizi ya ndani zaidi ya milioni 83.4 walioandikishwa mwaka uliopita, ni sawa na wakaazi wote wa Ujerumani, huku kukiwa na watu wengi wanaoyakimbia makaazi yao kutokana na migogoro kwenye maeneo kama vile Sudan na Gaza, pamoja na mafuriko na vimbunga vikali.
Mgongano wa matatizo
Mkuu wa IDMC, Alexandra Bilak amesema kuwa uhamiaji wa ndani hutokea wakati ambapo mizozo, umaskini na hali ya hewa vinagongana na kuwakumba walio hatarini zaidi.
Waangalizi hao wamesisitiza kuwa takribani asilimia 90 ya Wakimbizi wa Ndani ulimwenguni, au watu milioni 73.5, waliyahama makaazi yao kutokana na ghasia na mizozo, idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 80 tangu mwaka 2018.
Mkuu wa NRC, Jan Egeland, amesema takwimu za mwaka huu zinapaswa kuwa kama tahadhari, na hivyo kuhakikisha kuna mshikamano wa kimataifa. Egeland ameonya kuwa kukosekana kwa maendeleo kuelekea katika kudhibiti uhamiaji duniani, ni kutofaulu kwa sera na hali hiyo inasababisha doa la maadili kwa ubinaadamu.
Kulingana na ripoti hiyo, nchi zipatazo 10 kila moja ilirekodi zaidi ya wakimbizi milioni tatu wa ndani, kutokana na mizozo na ghasia mwishoni mwa mwaka 2024. Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan pekee vimesababisha wakimbizi wa ndani milioni 11.6, idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika nchi moja.
Karibu wakaazi wote wa Gaza hawana makaazi
Takribani watu milioni mbili, karibu wakaazi wote wa Ukanda wa Gaza, pia hawakuwa na makaazi mwishoni mwa mwaka 2024.
Ripoti ya IDMC na NRC, imeeleza kuwa ulimwenguni kote, karibu watu milioni 10 walihamishwa ndani ya nchi zao mwishoni mwa mwaka jana, baada ya kulazimika kukimbia kutokana na majanga, hiyo ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya miaka mitano iliyopita.
Aidha, wakimbizi wapya wa ndani milioni 65.8 walirekodiwa mnamo mwaka 2024, huku watu wengine wakilazimika kukimbia mara kadhaa katika mwaka huo huo.
Mizozo ilisababisha watu milioni 20.1 ikiwa ni idadi ya wakimbizi hao wapya walioyahama makaazi yao, huku rekodi ya watu milioni 45.8 ikiwa ni walioyakimbia makaazi yao kutokana na majanga.
Soma zaidi: IOM yazungumzia wakimbizi wa ndani Sudan
Matukio yaliyohusiana na hali ya hewa, mengi yakichochewa na mabadiliko ya tabianchi, yalisababisha asilimia 99.5 ya watu wote walioyakimbia makaazi yao mwaka uliopita.
Idadi ya nchi zinazoripoti mizozo na majanga ya watu wasio na makaazi imeongezeka kwa mara tatu zaidi katika kipindi cha miaka 15, huku zaidi ya robo tatu ya wakimbizi wa ndani wakiwa wamesababishwa na mizozo katika nchi wanazoishi ambazo zinakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi.
(AFP)