Watu kadhaa wauawa katika mapigano ya kaskazini mwa Mali
14 Juni 2025Vikosi vya usalama vya Mali vimepambana na wanachama wa kundi linalotaka kujitenga lenye silaha la Azawad kwa muda wa siku mbili, na kuwaua wanachama wake 10. Wanajeshi hao wanaotaka kujitenga wa Azawad, walisema pia kuwa wamewaua makumi ya wanajeshi wa Mali na wapiganaji wa kikosi chenye mafungamano na Urusi.
Mapigano hayo yalianza na mashambulizi ya kijeshi katika eneo la kaskazini mwa Mali la Kidal mnamo siku ya Alhamis. Msafara wa vifaa vya jeshi la Mali ulivamiwa siku ya Ijumaa kabla ya shambulio hilo kuzuiwa.
Vuguvugu hilo linalotaka kujitenga limekuwa likipigana kwa miaka kadhaa likitaka kuundwa kwa taifa la Azawad kaskazini mwa Mali. Wakati mmoja liliwahi kuvifurusha vikosi vya Mali katika eneo hilo kabla yamakubaliano ya amani ya mwaka 2015, ambayo hata hivyo yalivunjika.