Watu 82 wauwawa katika mashambulizi mapya ya Israel Gaza
21 Mei 2025Haya yamesemwa na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas na hospitali za eneo hilo.
Israel inaendeleza mashambulizi hayo licha ya ghadhabu za jumuiya ya kimataifa kwa kutanuliwa kwa mashambulizi hayo.
Inaarifiwa kwamba misaada iliyokubaliwa na Israel kuingia Gaza, bado haijawafikia Wapalestina walio katika hali ya kukata tamaa.
Haya yanajiri wakati ambapo Mamlaka ya Palestina imesema kundi moja la wanadiplomasia limeshambuliwa lilipokuwa katika ziara ya mji wa Jenin, ulioko Ukingo wa Magharibi.
Wanadiplomasia hao walikuwa katika ziara rasmi ya kutazama jinsi hali ya kiutu ilivyo, ndipo iliposikika milio ya risasi.
Jeshi la Israel limesema ziara hiyo ilikuwa imeidhinishwa, ila ujumbe wa wanadiplomasia hao ulipita njia tofauti na iliyokuwa imekubaliwa, ndipo wanajeshi hao wa Israel walipofyatua risasi ili kuwatahadharisha. Uhispania imelaani tukio hilo.