Watu 70 wauawa katika shambulio la hospitali Sudan
27 Januari 2025Takriban watu 70 wameuawa Sudan katika shambulio lililolenga hospitali pekee inayofanya kazi katika mji uliozingirwa wa El Fasher, hayo yamesemwa na Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus kwenye chapisho lake kwenye mtandao wa Kijamii wa X.
Hivi karibuni mapigano makali yameendelea katika mji wa El Fasher kati ya kundi la wapiganaji wa RSF na muungano wa vikosi vya jeshi la Sudan likiwemo jeshi lenyewe, polisi, makundi ya waasi na vikosi vya ulinzi vya eneo hilo.
Hospitali ya Saudi iliyoshambuliwa ndio hospitali pekee ambayo inafanya kazi katika mji huo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesema shambulio hilo limekiuka sheria za kimataifa.
Soma pia: Mapigano Sudan yasababisha moto kwenye kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO alikuwa wa kwanza kutoa taarifa hiyo kwamba watu 70 wameuawa na wengine 19 kujeruhiwa huku akiongeza kuwa kulikuwa na wagonjwa waliokuwa wakipatiwa huduma.
Tedros Ghebreyesus ametoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya huduma ya afya na wafanyakazi wake nchini Sudan na kuruhusu kutengenezwa kwa vifaa vilivyoharibiwa kutokana na shambulio hilo.
Shinikizo kubwa na majaribio ya upatanishi wa kimataifa ya kuumaliza mzozo huo nchini Sudan bado hayazaa matunda licha ya mataifa kama Marekani kutoa tathmini na kuwawekea vikwazo viongozi wa vikosi hivyo Jeneral Abdel Fatah Al Burhan wa jeshi la Sudan na Mohammed Hamdan Daglo wa RSF kwamba wanafanya mauaji ya kimbari.
Soma pia: Idadi ya waliouwawa Sudan katika shambulio hospitalini imefika watu 70
Tangu mwezi Mei 2024 mji wa El Fasher umekuwa chini ya mzingiro wa wapiganaji wa RSF na watoa huduma za kiutu wanasema wakaazi wa mji huo wamekuwa kwenye mateso kwa muda mrefu huku ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ukishuhudiwa.
Kwa upande wao RSF hawajatoa tamko lolote kufuatia shambulio hilo.
Burhan atembelea makao makuu Khartourm
Katika hatua nyingine, Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fatah Al Burhan ameutembelea hapo jana Jumapili makao makuu yake katika mji mkuu Khartoum, siku mbili baada ya vikosi kutwaa tena jengo hilo, ambalo wanamgambo wa RSF walikuwa wamezingira tangu vita vilipozuka Aprili 2023.
Akiwa kwenye makao hayo makuu Burhan amesema "watu wa Sudan wanaliunga mkono jeshi, na sote tunashuhudia jinsi wanavyotuunga mkono katika vita hivi. Vita hivi vinakaribia mwisho wake, na wapiganaji hawa wa Vikosi vya RSF watamalizika. Tunawaahidi watu wa Sudan kwamba tutaendelea kupigana hadi tufanikiwe''.
Tangu mwaka 2023 mzozo wao umeua zaidi ya watu 28,000, na kulazimisha mamilioni kuyakimbia makazi yao na kwadumbukiza mamailioni kwenye baa la njaa.