Watu 65 waliuawa kwenye maandamano ya Kenya, polisi lawamani
25 Julai 2025Katika ripoti hiyo iliyotolewa leo, IPOA imeeleza kuwa vifo vingi vilitokana moja kwa moja na hatua za polisi wakati wa operesheni za kudhibiti umati pamoja na matukio yaliyotokea wakati wa maandamano hayo. Mamlaka hiyo iliorodheshawaliojeruhiwa ambao ni aia 342 na maafisa wa polisi 171 kati ya Juni 17 hadi Julai 7, 2025.
Kuhusu vifo 65 vilivyoorodheshwa, IPOA imesema: "Huduma ya Polisi ya Kitaifa (NPS) iliitaarifu IPOA kuhusu vifo 5 pekee kati ya hivyo 65 vilivyobainishwa."
"Kukosa kuiarifu IPOA kuhusu vifo hivyo kunadhoofisha usimamizi huru, kunakiuka masharti ya kisheria ya utoaji taarifa, na ni dalili ya kutisha ya utamaduni wa kutozingatia sheria," imesema mamlaka hiyo.
Ripoti hiyo pia inaonyesha uharibifu mkubwa wa mali za umma na za watu binafsi wakati wa maandamano, ikiwa ni pamoja na kuchomwa kwa vituo vya polisi huko Kirinyaga, Nyandarua, na Nairobi, na uharibifu wa benki, maduka makubwa na majengo ya serikali katika kaunti za Meru, Embu, Kiambu, Nairobi, na Nakuru.
Serikali imewafungulia mashtaka ya ugaidi baadhi ya waandamanaji waliosababisha uharibifu wa mali za watu. Mkurugenzi wa afisi ya mashtaka ya umma nchini Renson Ingonga ametetea hatua hiyo inayopingwa na baadhi ya wanaharakati.
"Tunafanya maamuzi yetu wenyewe kwa kuzingatia sheria na ushahidi uliopo. Ugaidi sio tu unapotumia mabomu kulipua, bali ukifanya vitendo yanayohatarisha maisha ya umma na mitambo ya serikali, ni kitendo cha kigaidi ndiyo maana tunaweza kuwashtaki watu chini ya sheria hiyo."
Maandamano ya kutaka mageuzi
Katika ripoti hiyo, IPOA imebainisha kuwa waliwapelekwa maafisa wa polisi waliovaa sare na pia wasio na sare ili kudhibiti maandamano. Maafisa hao wote waliokuwa wakishughulikia maandamano hawakuvaa vibandiko vyenye majina yao na nambari za utambulisho kama inavyotakiwa na Ratiba ya Sita ya Sheria ya Kenya CAP 84.
Maafisa hao walikuwa wamejihami kwa bunduki, mabomu ya kutoa machozi, marungu na magari ya operesheni. Polisi walizuia watu kufika katika maeneo ya Harambee Avenue, Hazina ya Kitaifa, City Hall Way na Barabara ya Bunge kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.
Maandamano ya kwanza mwezi Juni 2025 yalifanyika tarehe 17 kufuatia kifo cha mwanablogu na mwalimu, Albert Ojwang', akiwa mikononi mwa polisi. Kifo chake kilisababisha ghadhabu kubwa kutoka kwa umma na kusababisha maandamano makubwa jijini Nairobi. Maandamano hayo yaliishia kwa tukio la raia Boniface Mwangi Kariuki kupigwa risasi kichwani na polisi, na baadaye kufariki hospitalini kutokana na majeraha yake.
IPOA ilieleza kuwa ilianzisha uchunguzi mara moja kuhusu kifo cha Kariuki, na uchunguzi huo ulisababisha kukamatwa kwa afisa mmoja wa polisi, Klinzy Masinde Barasa, ambaye tayari amefunguliwa mashtaka.
Wakati wa maadhimisho ya maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha (yanayoongozwa na kizazi cha Gen Z), Wakenya 23 walifariki. Kwa mujibu wa takwimu za IPOA, watu saba walifariki Nairobi, wanne Kiambu, wanne Nyeri, huku Machakos na Makueni wakirekodi vifo viwili kila mmoja. Kaunti za Uasin Gishu, Kajiado, Nyandarua na Nakuru ziliripoti kifo kimoja kila moja.
Mauwaji yalitokea maeneo mengi
Siku hiyo hiyo, raia 195 na maafisa wa polisi 99 walijeruhiwa. Watu 362 walikamatwa katika maeneo mbalimbali ambapo maandamano yalikuwa yanaendelea. Mamlaka hiyo pia ilirekodi vifo 41 wakati wa maandamano ya saba saba, Julai 7, 2025.
Kwa mgawanyo wa vifo kulingana na maeneo: Nairobi (7), Kiambu (10), Kajiado (7), Nakuru (3), Nyandarua (1), Meru (2), Embu (3), Kirinyaga (1), Laikipia (3) na Murang'a (4).
Rais William Ruto amekuwa akiitetea mara kwa mara huduma ya polisi na hatua zao, hata akiwahi kusema kuwa waandamanaji wenye fujo wanastahili kupigwa risasi miguuni. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wanaopinga sera zake wanatoa wito wa kusitisha mauaji. Boni Khalwale ni Seneta wa Kaunti ya Kakamega.
Ripoti hiyo inaonyesha kwa upana ukiukaji wa viwango vya kikatiba vya uendeshaji wa shughuli za kipolisi na kushindwa kulinda usalama na haki za umma. Ili kukabiliana na hali hiyo, IPOA imetoa wito wa kufanyika kwa mageuzi ya dharura ndani ya idara ya polisi.