Watu 64 wauawa Gaza kwa mashambulizi ya Israel
16 Mei 2025Hayo ni katika wakati shinikizo linaongezeka kwa Israel kufungua njia za kupelekwa misaada ya kiutu kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina.
Shirika la Huduma za Kiraia la Ukanda wa Gaza limesema Israel imeyalenga makaazi ya watu upande wa kaskazini na kusababisha idadi hiyo ya vifo na kuwajeruhi makumi wengine ikiwemo wanawake na watoto.
Hayo yamearifiwa wakati Marekani iliyo mshirika wa karibu wa Israel, imeelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya hali ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza. Rais Donald Trump amekiri kwa mara kwanza kwamba watu wa Gaza "wanataabika kwa njaa" na kuahidi kuwa Washington "inafuatilia kwa karibu hali hiyo na itaishughulikia".
Katika siku za hivi karibuni mashirika kadhaa ya kimataifa yameonya kuwa ukosefu wa chakula kwenye eneo hilo umefikiwa kiwango kisicho mithili na kutoa rai kwa Israel iruhusu misaada ya kiutu kuingia kwa wingi ndani ya Ukanda wa Gaza.