Watu 50 wauawa nchini Kongo baada ya kushambuliwa na ADF
9 Septemba 2025Afisa wa serikali katika eneo hilo Macaire Sivikunula amesema shambulio hilo limetokea jana usiku katika kijiji cha Ntoyo, kilichopo katika eneo la Lubero, jimbo la Kivu Kaskazini.
Msimamizi wa kijeshi wa Lubero Kanali Alain Kiwewa, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba, idadi ya watu waliouawa ni takriban watu 60 na huenda ikaongezeka kwani baadhi ya watu bado hawajapatikana.
Kundi la ADF ni miongoni mwa makundi kadhaa ya waasi yanayopigania ardhi na raslimali katika eneo la mashariki mwa Kongo, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Jeshi la serikali ya Kongo kwa kushirikiana na Uganda, limeeleza kwamba limeimarisha oparesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la ADF katika wiki za hivi karibuni.
Mwezi uliopita, kundi la ADF liliwaua zaidi ya watu 50 huku likiwaua watu wengine 38 katika shambulio tofauti la kanisa mnamo mwezi Julai.