Watu 5 wameuawa kwenye mapigano kati ya Kongo na Wazalendo
28 Agosti 2025Matangazo
Duru za kijeshi zimeeleza kuwa mapigano hayo yalizuka siku ya Jumanne katika mpaka wa Kavimvira, karibu na Uvira.
Msemaji wa jeshi la Kongo katika jimbo la Kivu Kusini, Reagan Mbuyi Kalonji amesema waliouawa katika mapigano hayo ni wapiganaji watano wa Wazalendo, na mwanajeshi mmoja wa Kongo alikuwa miongoni mwa watu wawili waliojeruhiwa.
Kwa mujibu wa Kalonji, mapigano hayo yalichochewa na mivutano ya kikabila.
Vyanzo vya kiusalama vimeeleza kutokea kwa mapigano makali katika siku za hivi karibuni kwenye jimbo la Kivu Kusini kati ya waasi wa M23, jeshi la Kongo na washirika wake Wazalendo.
Jeshi la Kongo linahofia kwamba M23 linajiandaa kwa mashambulizi mapya katika eneo la Uvira.