Watu 46 wameuwawa katika ajali ya ndege Sudan
26 Februari 2025Ndege hiyo aina ya Antonov ilianguka siku ya Jumanne usiku karibu na kambi ya jeshi ya Wadi Seidna, moja wapo ya vituo vikubwa zaidi vya jeshi la anga katika eneo la Omdurman, kaskazini magharibi mwa Khartoum.
Jeshi la Sudan ambalo limekuwa likipigana na wanamgambo wa RSF tangu April 2023, limesema ndege hiyo ilianguka wakati wa kuruka na kusababisha vifo na kujeruhia wanajeshi na raia.
Taarifa ya mamlaka ya mji wa Khartoum imesema baada ya tahmini ya mwisho idadi ya walipoteza maisha ilifikia 46 huku wengine 10 wakijeruhiwa.
Hapo awali wizara ya afya Sudan iliripoti vifo vya watu 19 na kuongeza kwamba kikosi cha dharura kiliwakimbiza hospitalini majeruhi wakiwemo watoto.
Soma pia:Kundi lenye silaha lauwa wanakijiji 26 Sudan
Mashahidi wanasema kulisikika mlipuko mkubwa na nyumba kadhaa ziliharibiwa katika eneo hilo la mkasa, huku huduma ya umeme ikatika katika maeneo ya karibu. Chanzo cha kijeshi kimetaja hitilafu za kiufungi kuwa chanzo cha ajali hiyo.
Itakumbukwa kwamba ajali hiyo imetokea siku moja baada ya wanamgambo wa RSF kudai kuidungua ndege nyingine ya kijeshi iliyotengenezwa Urusi aina ya Ilyushin, katika anga la Nyala kwenye mji mkuu wa Darfur kusini. Wanamgambo wa RSF walisema ndege hiyo iliharibiwa ikiwa na wahudumu wake wote ndani.
Vyombo vya habari nchini Sudan vinaripoti kwamba, ndege hiyo iliyokuwa imebeba maafisa wa ngazi za juu wa jeshi ilikuwa ikielekea katika mji wa Port Sudan ambao ni makao ya serikali inayoungwa mkono na jeshi. Hata hivyo jeshi la Sudan halijathibitisha juu ya taarifa hizo.
Usalama wa anga Sudan
Sudan imekuwa na rekodi mbaya ya usalama wa anga ambapo ajali za ndege zimekuwa zikitokea mara kwa mara.
Mnamo mwaka 2020 takriban watu 16 walipoteza maisha baada ya ndege ya jeshi aina ya Antonov An-12 iliyotengenezwa Urusi kuanguaka katika mkoa wa Darfur.
Rekodi zinaonesha pia mnamo mwaka 2003 ndege ya shirika la ndege la Sudan ilianguka kwenye vilima wakati ikijaribu kutua kwa dharurua, na kuuwa watu takriban 116 wakiwemo raia kutoka nje ya Sudan, huku mtoto mmoja wa kiume akinusurika katika mkasa huo.
Soma pia:Sudan yaishutumu Kenya kwa kuruhusu mazungumzo ya RSF
Vita vya wenye kwa wenyewe vinavyoendelea Sudan vimeharibu maeneo ya mijini na kuhusisha uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na ubakaji na mauaji ya kikabila. Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu yamelaani vikali vitendo hivyo.
Jeshi linapambana kurudisha udhibiti wa mji wa Khartoum na maeneo mengine kutoka kwa RSF, ambayo inadhibiti sehemu kubwa ya Darfur.
Mwishoni mwa juma, RSF ilisaini mkataba na washirika wa kisiasa na makundi yanayomiliki silaha mjini Nairobi, Kenya, hatua inayonuwiya kuunda serikali mbadala katika maeneo wanayoyadhibiti.