Watu 400,000 wamelazimika kuyahama makazi yao nchini Kongo
24 Januari 2025Akizungumza na waandishi wa habari akiwa mjini Geneva, msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Matthew Saltmarsh, amesema idadi ya watu waliohamishwa kutokana na vita hivyo ni zaidi ya watu 400,000 mwaka huu pekee, karibu mara mbili ya idadi iliyoripotiwa wiki iliyopita.
Mapigano yanaendelea katika mji wa Sake kilomita 20 tu kutoka Goma, huku chanzo cha usalama kikitoa taarifa kwa sharti la kutotajwa jina, kikieleza kwamba mapambano pia yanaendelea katika eneo la Kanyamahoro Kibumba.
Uturuki yajitolea kuwa mpatanishi katika vita vya DRC
Haya yanajiri huku Rais wa Kongo Felix Tshisekedi akitarajiwa kufanya mkutano wa baraza la ulinzi. Kulingana na vyanzo vya kijeshi na Umoja wa Mataifa, Gavana wa kijeshi wa Kivu Kaskazini, Jenerali Peter Cirimwami, amefariki leo asubuhi, baada ya kupigwa risasi katika mstari wa mbele wa mapambano hapo jana.