Watu 40 wafariki kutokana na kipindupindu Sudan
14 Agosti 2025Katika kubabiliana na hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo, maafisa wa afya nchini Sudan wamezindua kampeni ya siku 10 ya chanjo ya kipindupindu katika mji mkuu, Khartoum, ili kuzuia mlipuko zaidi wa ugonjwa huo. Lilian Mtono na taarifa zaidi.
Taarifa ya Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imesema eneo kubwa la magharibi, linalokabiliwa na mapigano kwa zaidi ya miaka miwili kati ya jeshi la serikali na Vikosi vya RSF, ndilo limeathiriwa zaidi.
MSF imesema, vita hivyo na ukosefu wa maji safi ndio sababu ya raia wengi kuhama.
Vifo zaidi ya elfu mbili vya kipindupindu
Wiki iliyopita madaktari hao wasio na mipaka waliarifu kuwatibabu wagonjwa wa kipindupindu zaidi ya 2,300 huku ikisema zaidi ya wagonjwa 40 walipoteza maisha.
Shirika hilo la madaktari limeongeza kuwa kati ya mwaka 2024 mpaka August 11 mwaka huu vifo takriban 2,470 vinavyohusiana na kipindupindu vimeorodheshwa miongoni mwa wagonjwa 99,700 wanaohusishwa na kipindupindu nchini Sudan.
"Hali ni mbaya zaidi huko Tawila, jimbo la Darfur Kaskazini, ambapo watu 380,000 wamekimbia mapigano yanayoendelea karibu na mji wa El-Fasher, kulingana na Umoja wa Mataifa,"mwisho wa kunukuu, imesomeka sehemu ya taarifa ya madakati wasio na mipaka wanaotoa huduma huko Sudan
Katika kubabiliana na hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo, maafisa wa afya nchini Sudan wamezindua kampeni ya siku 10 ya chanjo ya kipindupindu katika mji mkuu, Khartoum, ili kuzuia mlipuko zaidi wa ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine, shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP limesema maeneo 17 nchini Sudan ikiwemo Darfur, Milima ya Nuba, Khartoum na Kazira nchini Sudan yamo hatarini kukumbwa na baa la njaa na kutoa wito wa hatua za haraka za misaada ya kubinadamu ili kuyanusuru maeneo hayo na madhila ya njaa.
Ufadhili wa fedha kwa maelfu ya watu
Msemaji wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Guterres, Stéphane Dujarric, amesema tayari Shirika hilo(WFP), limetoa wito wa misaada zaidi ya kibinadamu hasa katika jimbo la El Fasher, linalokabiliwa na njaa kubwa.
"Washirika wetu wa WFP wametoa wito wa upatikanaji wa misaada katika jimbo la El fasher linalokabiliwa na njaa kubwa na ambalo sio rahisi kufikishiwa misaada. WFP imesema baadhi ya wakaazi katika jimbo hilo wanaishi kwa kula majani yanayoliwa na wanyama na mabaki ya vyakula," alisema Dujarric.
Shirika hilo la Mpango wa Chakula Duniani(WFP), linaendelea kuwafadhili kifedha takriban robo milioni ya watu kuwawezesha kununua vyakula ambavyo pia vinaendelea kupungua kwenye masoko.