Mkimbizi wa Afghanistan agonga waandamanaji Ujerumani
13 Februari 2025Mashahidi waliripoti hali ya machafuko mara baada ya tukio, huku watu wakilia, wakitetemeka, na wakiwa na majeraha makubwa. Mmoja alionekana amelala chini ya gari, huku mwingine akiondolewa na polisi baada ya madai kwamba maafisa walirusha risasi kwenye dirisha la gari hilo.
Watoa huduma za dharura, wakiwemo wahudumu wa afya na mashirika ya ulinzi wa kiraia, waliwasili haraka eneo la tukio.
Soma pia: Gari lagonga watu Ujerumani, watatu wauawa, 20 wajeruhiwa
Vitu kama miwani, viatu, mablanketi, na hata baiskeli za walemavu vilitapakaa katika eneo hilo, ishara ya athari kubwa ya ajali hiyo. Msemaji wa idara ya zimamoto, Bernhard Peschke, amethibitisha kuwa baadhi ya waathirika wako katika hali mbaya inayohatarisha maisha yao, huku watoto wakiwa miongoni mwa majeruhi.
"Kwa sasa, tunakadiria kuwa takribani watu 20 wamejeruhiwa, baadhi yao vibaya, na wanahudumiwa na mashirika ya misaada na kikosi cha zimamoto.
Idadi kamili ya majeruhi bado haijathibitishwa, kwani wengine wenye majeraha madogo wameelekea majengo ya jirani. Hatuwezi pia kuondoa uwezekano wa hatari kwa maisha yao," alisema Peschke.
Dereva atambuliwa, uchunguzi waendelea
Msemaji wa polisi Munich ametambua dereva wa Mini Cooper kuwa ni muomba hifadhi wa miaka 24 kutoka Afghanistan.
Soma pia:Ujerumani: Gari laparamia watu soko la Krismasi mjini Magdeburg
Waziri Mkuu wa Bavaria, Markus Söder, amesema shambulio hilo linashukiwa kuwa la makusudi, huku Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, akisisitiza kuwa mtuhumiwa lazima akabiliane na sheria, ikiwemo kufukuzwa nchini.
Polisi imethibitisha kuwa dereva huyo amekamatwa na siyo tishio tena, huku uchunguzi ukiendelea kubaini ikiwa alilenga waandamanaji kwa makusudi au ikiwa ilikuwa hitilafu ya breki.
Tahadhari zaidi za usalama
Maafisa wa Munich wameelezea mshtuko wao kuhusu tukio hilo. Meya wa jiji, Dieter Reiter, alieleza wasiwasi wake mkubwa na kutuma salamu za pole kwa waliojeruhiwa.
Tukio hili linazidisha tahadhari za kiusalama, hasa wakati ambapo Munich inajiandaa kwa mkutano wa ngazi ya juu wa usalama katika Hoteli ya Bayerischer Hof, takriban kilomita 1.6 kutoka eneo la tukio, siku moja tu baada ya shambulio hilo.
Mkutano huo unatazamiwa kuwavutia viongozi waandamizi wa dunia, akiwemo Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, katikati ya maandalizi ya uchaguzi ujao wa Februari 23 na mashambulizi ya hivi karibuni ya vurugu katika maeneo tofauti ya Ujerumani.
Soma pia: Waziri Faeser asema AfD haipaswi kujinufaisha na tukio la Magdeburg
Wakati uchunguzi ukiendelea, tukio hilo linasalia chini ya darubini kali, kutokana na muda wake na athari zake kwa usalama wa mkutano wa kimataifa na kipindi cha uchaguzi wa kitaifa.