Watu 23 wauawa, 20 wachukuliwa mateka Kongo
1 Machi 2025Vyanzo vya habari kwenye eneo hilo vimeliambia shirika la habari la AFP kwamba waasi wa kundi la ADF walivamia jimbo la Ituri linalopakana na Uganda siku za Jumanne na Jumatano na kufanya uhalifu huo.
Jospin Paluku, mratibu wa asasi za kijamii katika eneo la Mambasa amesema idadi hiyo ni ya awali wakati wakikusanya taarifa zaidi za walioathirika na mkasa huo, akiongeza kuwa mmoja wa waliochukuliwa mateka ni mtoto wa kiume wa chifu wa eneo hilo.
Soma zaidi: Waasi wa ADF waushambulia mji wa Beni
Idadi hiyo imethibitishwa na makundi ya haki za binaadamu yaliyosema wengi wa waliouawa na kuchukuliwa mateka ni wakulima waliokuwa mashambani.
Kundi la ADF linaloundwa na waasi kutoka Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake kaskazini mashariki mwa Kongo tangu katikati mwa miaka ya 1990.
Maelfu ya raia wameuawa kutokana na uasi huo licha ya kutumwa wanajeshi wa Uganda kupambana na kundi hilo.