Watu 23 waliotaka kuwa aksari wauwawa Iraq
23 Januari 2006Machafuko ya umwagaji damu nchini Iraq yanazidi kupamba moto leo hii watu wawili wameuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio la kujitolea muhanga maisha nje ya ubalozi wa Iran mjini Baghdad.
Kugunduliwa kwa maiti hizo kunaonyesha jinsi gani ilivyo rahisi kushambuliwa kwa watu wanaotaka kuwa askari polisi na kunakuja wakati vyama vya kisiasa vikiwa vimeanza kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita vikilalamika kwamba ulihujumiwa.
Maiti zao ni sehemu ya kundi la watu 35 waliokuwa wakitaka kujitolea kuwa askari polisi ambao walikuwa hawajulikani walipo tokea Jumatatu iliopita na zilipatikana katika ardhi ya uwanda karibu na Nabaie maili chache kutoka mji mkuu wa Baghdad. Mikono yao ilikuwa imefungwa na waliuwawa kwa kupigwa risasi.
Watu hao walikuwa wametokea Samarra kilomita 125 kaskazini mwa Baghdad na walikwenda mjini humo kutaka kujiunga na polisi lakini walikataliwa na walikuwa wakirudi nyumbani wakati walipokumbwa na maafa hayo.
Wakati huo huo raia wa Jordan anayeshikiliwa mateka nchini Iraq amesema kwenye ukanda wa video uliorushwa na televisheni ya Al Arabiya kwamba watu waliomteka wamemfunga na ukanda wa mabomu na kuweka siku nne za mwisho za kumuuwa venginevyo madai yao yanatimizwa.
Mtu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mahmud Salman Saadiyat alikuwa dereva wa ubalozi wa Jordan nchini Iraq na alitekwa nyara kusini mwa Baghdad hapo tarehe 20 Desemba ameitaka serikali ya Jordan kutopuuza kilio chake kutokana na maisha yake kuwa hatarini.
Hii ni mara ya nne kwamba watekaji wake wameongeza muda wa kutaka kumuuwa kwa kusema kwamba atauwawa venginevyo mwanamke wa Kiiraq Sajida al Rishawi anaachiliwa huru kutoka gerezani ambako amekuwa akishikiliwa tokea kuripuliwa kwa mabomu mjini Amman Jordah hapo mwezi wa Novemba.
Ukanda huo wa video unakuja huku kukiwa na ongezeko la wasi wasi juu ya mwandishi wa habari wa Marekani aliyetekwa nyara Jill Caroll ambaye watekaji wake wametishia kumuuwa venginevyo wanajeshi wa Marekani wanawaachilia huru wanawake wote wa Iraq wanaoshilikiwa gerezani nchini Iraq.
Afisa wa wizara ya sheria nchini humo amesema kwamba wanawake hao sita wa Iraq walioko mahabusu wataachiliwa huru na jeshi la Marekani katika kipindi kisichozidi wiki moja.
Machafuko ya umwagaji damu yanaendelea bila kusita nchini Iraq hapo jana watu 11 wameuwawa wakiwemo askari polisi na kiongozi wa manispaa wa Kishia pamoja na watoto wanne.
Takriban watu wawili wameuwawa leo hi na wengine watano kujeruhiwa wakati wa shambulio la kujitolea muhanga maisha kwa kutumia gari lililotegwa mabomu dhidi ya doria ya polisi nje ya ubalozi wa Iran mjini Baghdad.
Picha za teleivisheni ya Iraq zimeonyesha gari la polisi lililoteketea na watu kadhaa waliojeruhiwa wakiondolewa kwenye eneo la tukio hilo.Televisheni hiyo pia imeonyesha mguu wa mtu ukiwa katikati ya barabara na mabaki ya askari polisi alieyeteketezwa yakiwa ndani ya gari.
Katika vurugu nyengine raia wanne wamejeruhiwa katika shambulio la bomu lililotegwa kwenye gari karibu na jengo la mhakama huko Mahmudiya kusini mwa Baghdad na askari polisi watano wamejeruhiwa katika shambulio la bomu kwenye mji wa kusini mwa Kirkuk.
Wakati machafuko yakiendelea vyama vya kisiasa nchini Iraq vina siku mbili za kupinga matokeo yasiyoyakinishwa rasmi yaliotangazwa hapo Ijumaa kufuatia uchaguzi mkuu wa tarehe 15 Desemba ambao ni wa kwanza kuchaguwa bunge la kudumu kufuatia kuangushwa kwa Saddam Hussein hapo mwaka 2003.
Katika wiki zinazokuja kunatarajiwa kushuhudiwa kwa mazungumzo magumu na majadiliano makali yatakayochukuwa muda mrefu ya kuunda serikali ya kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka minne ijayo mchakato ambao wachunguzi wa mambo wanasema unaweza kuchukuwa hata miezi miwili kukamilika.
Ingawa vyama vyote vikuu vimelalamikia matokeo hayo ukiwemo Muungano wa Umoja wa Iraq wa kundi la Washia uliojisombea viti 128 kati ya viti 275 vya bunge hakuna chama kilichoukataa mchakato wa uchaguzi kwa ujumla na vyote vinaonekana kuwa viko tayari kujiunga na mazungumzo ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.