Watu 22 wauwawa kwa mashambulizi ya Israel mjini Gaza
25 Mei 2025Msemaji wa taasisi ya ulinzi wa raia Mahmud Bassal, amesema watu saba waliuwawa katika shambulizi hilo lililolenga jumba moja mjini Jabalia Kaskazini mwa Gaza.
Bassal amesema wanahofia watu wengine bado wamenasa chini ya vifusi vya jengo hilo lililoporomoka na kuongeza kuwa taasisi yake haina vifaa vya kutosha kuwaokoa au hata kutoa maiti zilizoko chini ya vifusi hivyo.
Watu wengine wawili akiwemo mwanamke aliyekuwa na mimba ya miezi saba, waliuwawa pia katika shambulio lililolenga makambi yaliyowahifadhi watu waliokosa makazi karibu na eneo la Nuseirat katikati ya Gaza.
Netanyahu awakosoa viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Canada
Haya yanaripotiwa wakati Jeshi la Israel likitangaza kudungua kombora lililorushwa nchini mwake na waasi wa Houthi wa Yemen. Hakuna ripoti zozote hadi sasa za majeruhi au uharibifu wowote wa majengo.
Waasi hao wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wamekuwa wakiishambulia Israel kwa makombora wakisema wanafanya hivyo kupinga mashambulizi yanayofanywa na taifa hilo dhidi ya wanamgambo wa Hamas mjini Gaza.