Watu 22 wapotea katika ghasia za wavuvi wa Kenya na Ethiopia
24 Februari 2025
Takriban watu 22 hawajulikani walipo baada ya a mapigano yaliyotokea kwenye eneo la mpaka kati ya wavuvi wa Ethiopia na Kenya, hii ikiwa ni kulingana na Polisi wa Kenya na maafisa wa serikali.
Gavana wa kaunti ya Turkana nchini Kenya Jeremiah Lomorukai amesema jana Jumapili kwamba mapigano hayo yalitokea Jumamosi jioni huko Lopeimukat na Natira karibu na mto Omo kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia.
Soma: Kina cha maji katika Ziwa Turkana Kenya kimeongezeka
Polisi wa kaunti ya Turkana walisema jana kwamba karibu wavuvi wa Kenya 22 hawakujulikana waliko, na boti 15 ziliibiwa; wakati wavuvi sita wa kabila la Dasenech kutoka Ethiopia wakiokolewa na kurudi nchini kwao.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen aliandika kupitia X jana Jumapili kwamba serikali imeimarisha ulinzi kwenye eneo hilo la mpaka na kushirikiana na Addis Ababa kufikia makubaliano ya amani kati ya jamii hizo mbili.