Watu 17 wauawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
23 Julai 2025Msemaji wa shirika la ulinzi wa raia huko Gaza Mahmoud Bassal amesema watu wanane akiwemo mjamzito wameuawa katika kitongoji cha Tel Al-Hawa na wengine waliuawa katika mji wa kusini wa Bani Suheila na kituo cha usambazaji wa chakula katikati mwa Gaza.
Jeshi la Israel limedai kuwa operesheni hiyo ilikuwa ikiwalenga wanamgambo wa Hamas. Siku ya Jumatano, zaidi ya mashirika 100 ya misaada ya kibinadamu yameonya kuhusu hatari ya kuenea kwa njaa huko Gaza, huku mkuu wa hospitali ya Al-Shifa akisema kwamba watoto 21 wamekufa kutokana na utapiamlo katika muda wa siku tatu zilizopita.
Israel inakabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea Gaza, ambako zaidi ya watu milioni mbili wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na mahitaji muhimu, lakini Israel imekuwa ikikanusha kuzuia usambazaji wa misaada ya kiutu.