Mashambulizi ya Urusi yawaua watu 14 Ukraine
28 Agosti 2025Mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine usiku wa kuamkia Alhamisi ndiyo makubwa baada ya wiki kadhaa wakati kukiwa na juhudi zinazoongozwa na Marekani za kuvimaliza vita kati ya Moscow na Kyiv. Katika mashambulizi hayo Ukraine imesema imeshambuliwa kwa droni takriban 598 na makombora 31 ya aina mbalimbali kote nchini humo kulingana na jeshi la anga la Ukraine.
Miongoni mwa waliouwawa katika mashambulizi hayo ya Urusi ni watoto watatu wa miaka 2, 14 na 17 kwa mujibu wa mamlaka za Kyiv. Timu za uokoaji zimepelekwa katika maeneo yaliyoshambuliwa ili kuwanasua watu walionasa chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka.
Akizungumzia mashambulizi hayo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine Ihor Klymenko amesema, "Idadi ya watu walioathirika itaongezeka kwa kuwa tuna ripoti kwamba watu saba waliokuwa kwenye jengo hili hawajapatikana. Droni ililenga ghorofa ya tatu na ya nne. Kati ya waliokufa hapa Kyiv ni mtoto mwenye miaka 14 na mtoto mwingine mwenye miaka 11 ana hali mbaya na yuko hospitali. Karibu watu 40 wamejeruhiwa mjini Kyiv."
Ofisi za Umoja wa Ulaya Kyiv zashambuliwa
Naye Rais wa Halmashauri Kuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen kupitia ukurasa wake wa X ameyalaani mashambulizi hayo na kuongeza kuwa kuwa jengo la ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Kyiv limeathiriwa lakini wafanyakazi wake wako salama. Kamishna wa umoja huo Marta Kos amelilaani pia shambulio hilo lililofanywa na Moscow.
Kwa upande wake Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema mifumo yake ya anga imezidungua droni 102 za Ukraine. Katika mashambulizi hayo Kyiv imesema iliilenga mitambo ya kusafisha mafuta ya Afipsky na Kuybyshevskyi. Droni za Ukraine zimekuwa zikiilenga miundombinu ya mafuta katika wiki za hivi karibuni kwa madhumuni ya kuudhoofisha uchumi wa Urusi.
Mashambulizi ya Ukraine ambayo yameshailenga mitambo 10 ya mafuta imedhoofisha asilimia 17 ya uwezo wa uzalishaji wa mitambo hiyo sawa na mapipa milioni 1.1 ya mafuta kwa siku.