Watu 14 wajeruhiwa maandamano ya upinzani Msumbiji
6 Machi 2025Mamia ya wafuasi wa upinzani walijiunga kwenye msafara wa Mondlane kuzunguka mji mkuu Maputo, ikiwa ni mojawapo ya shughuli alizoandaa kote nchini humo kukitambulisha chama chake kipya cha siasa.
Hata hivyo inaarifiwa polisi ilitumia risasi za moto na gesi ya kutoa machozi kuusambaratisha mkusanyiko huo. Mratibu wa asasi ya kiraia inayofuatilia shughuli za kisiasa nchini Msumbiji ya Plataforma Decide amethibitisha watu 14 wamejeruhiwa kwenye vurumai hiyo ikiwemo watoto wawili.
Mondlane alishika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa rais uliofanyika Oktoba mwaka jana kwa kupata asilimia 24 ya kura.
Hata hivyo mwanasiasa huyo aliyapinga matokeo hayo akisema yalikuwa ya wizi na akaitisha mfululizo wa maandamano ya umma yaliyokabiliwa kwa nguvu ya vyombo vya dola na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 320.