Watu 13 wauawa katika shambulizi la kujitoa mhanga Mogadishu
18 Mei 2025Polisi imesema mshambuliaji aliingia katika kambi ya kijeshi na kujilipua miongoni mwa vijana kama 200 waliokuwa wakitaka kusajiliwa jeshini.
Soma pia: Somalia na Ethiopia kurejesha uhusiano wa kidiplomasia
Kundi la kigaidi la al-Shabaab limedai kuhusika na shambulizi hilo. Polisi imesema watu wengine 16 wamejeruhiwa na idadi ya waliokufa inatarajiwa kuongezeka. Mlio wa mlipuko huo ulisikika katika maeneo kadhaa ya mji huo mkuu. Al-Shabaab imedai kupitia kituo chao cha redio kuwa imewaua makuruta kadhaa wapya wa jeshi la Somalia.
Kundi hilo lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limeituhumu serikali kwa kuwatumia vibaya vijana wasio na ajira kwa kuwatuma kupigana na wanamgambo hao. Al-Shabaab imekuwa ikifanya mashambulizi nchini Somaliana nje ya nchi hiyo kwa miaka mingi ikitaka kuanzisha dola linalofuata sharia za Kiislamu.