Watu 12 wauawa na shambulizi la Marekani nchini Yemen
21 Aprili 2025Wizara ya afya ya waasi wa Houthi imesema mapema leo kwamba mashambulizi ya kutokea angani yaliyofanywa na Marekani katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, yamewaua watu wapatao 12 na kuwajeruhi wengine 30.
Shirika la habari linaloendeshwa na waasi wa Huthi, Saba, limeinukulu wizara hiyo ikisema vifo na majeraha yalitokana na mashambulizi ya usiku kucha yaliyofanywa na adui Mmarekani katika soko na eneo la makazi katika wilaya ya Farwa mjini Sanaa.
Shirika la habari la Saba limesema mashambulizi mengine yaliripotiwa jana Jumapili katika mkoa wa kati wa Marib, mkoa wa Hodeida upande wa magharibi na ngome ya Wahuthi ya Saada upande wa kaskazini.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Jumamosi iliyopita kwamba ana wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi hayo ya Marekani, lakini pia akawata Wahuthi wakome kufanya mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel na safari za meli katika eneo la Ghuba.