Watoto 21 wafariki kwa utapiamlo Gaza
22 Julai 2025Mkuu wa hospitali ya Al Shifaa katika Ukanda wa Gaza, Mohammed Abu Salmiya amesema watoto 21 wamekufa katika maeneo mbalimbali ya Ukanda huo, kutokana na utapiamlo na njaa katika kipindi cha saa 72 zilizopita.
Taarifa hizo zimetolewa katika wakati Israel imeendelea kushinikizwa na kukosolewa kimataifa kuhusu madhila inayoyasababisha kwenye Ukanda waGaza.
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, ametahadharisha hivi leo kwamba, operesheni za kijeshi za Israel zilizoongezeka Gaza zinasababisha kitisho kikubwa cha kuvunjwa kwa sheria ya kimataifa.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amemwambia mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Israel, Gideon Saar,kwamba Israel inapaswa kusitisha mauaji ya raia wasiokuwa na hatia wanaotafuta msaada.
Rais wa Uturuki, Recep Erdogan, katika hotuba yake mjini Istanbul,leo amesema haikubaliki kuona Wapalestina wakipoteza maisha kwa sababu ya kutafuta riziki.