Watawala wa kijeshi Sahel kutoa fursa kwa wazawa
7 Aprili 2025Nchini Niger, kampuni ya ndani imepewa leseni ya kuchimba shaba na huku serikali za kijeshi nchini Mali na Burkina Faso zinalenga kupunguza utegemezi kwa makampuni ya kigeni ya uchimbaji madini na kubadilisha uchumi wao.
Niger inataka kukuza uchumi wake na kupanua sekta yake ya madini kwa kuchimba shaba katika eneo la Agadez. Nchi hiyo imetoa kibali kwa kampuni ya kitaifa ya Compagnie Miniere de l'Air (Cominair SA).
Kulingana na taarifa kutoka kwa serikali ya kijeshi ya Niger, ambayo ilichukua mamlaka kufuatia mapinduzi ya Julai 2023, "Niger inaendelea na mpango wake wa kuleta mseto wa uzalishaji wa madini" kwa hatua ambayo "inaashiria kuingia kwake katika mtandao wa nchi zinazozalisha madini hayo kimkakati".
Soma pia:Mali, Burkina Faso na Niger zakataa kujiunga tena na ECOWAS
Ulf Laessing, mkuu wa mpango wa kikanda wa Sahel katika Wakfu wa Konrad Adenauer katika nchi jirani ya Mali, amesema makubaliano hayo ni sehemu ya mkakati wa Niger kupunguza utegemezi wake kwa makampuni ya kigeni kwa uchimbaji wa madini.
Laessing amesema kuwa haiwezekani kutabiri jinsi mradi huo utakavyofanikiwa kwa sababu "Mgodi wa shaba uko kaskazini, sio mbali na Libya, ambapo hali ya usalama ni mbaya sana."
Amesema kuwa Niger inafuata mwelekeo unaoonekana nchini Burkina na Mali, ambapo serikali za kijeshi zinategemea zaidi makampuni ya ndani, badala ya kutegemea za mataifa ya Magharibi.
Waendeshaji wa mgodi huo ulioko katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Niger, Moradi, wanatarajia kuzalisha wastani wa tani 2,700 za shaba kwa mwaka katika kipindi cha miaka kumi.
Niger yatumai kupunguza changamoto ya ajira
Serikali ya Niger inatumai kuwa mgodi huo utatoa fursa ya mamia ya ajira mpya na biashara yenye faida kubwa. Kwa sasa shaba inauzwa kwenye soko la dunia kwa $9,700 (€8,789) kwa tani.
Wakati huo huo, kibali cha muda kimetolewa kwa kampuni ya Niger Compagnie Miniere de Recherche et d'Exploitation (Comirex SA) huko Dannet ili kuzalisha lithiamu, kiungo muhimu cha betri za lithiamu zinazoweza kuchajiwa tena na ambazo huendesha kila kitu kutoka kwa simu za rununu hadi magari ya umeme.
Kampuni hiyo inatarajia kuzalisha tani 300 za lithiamu kwa mwaka. Niger ina hisa 25% katika mgodi wa shaba wa Cominair na hisa 40% katika kampuni ya Comirex ili kudumisha udhibiti wa serikali juu ya rasilimali za taifa hilo.
Soma pia:Utawala wa kijeshi wa Niger wawaachia mawaziri wa serikali iliyopinduliwa
Laessing ameiambia DW kuwa chanzo cha fedha kwa ajili ya miradi ya uchimbaji madini hakiko wazi, na kwamba huenda uchimbaji wa shaba unafadhiliwa kwa kiasi na mapato ya uzalishaji wa mafuta.
Mtawala wa zamani wa kikoloni wa Niger, Ufaransa, amepoteza umaarufu katika eneo la Sahel na amepoteza ushawishi.
Jeshi la Niger halijioni tena kuwa limefungwa na mikataba ya ushirikiano kutoka kwa Rais wa Niger Mohamed Bazoum, ambaye alitimuliwa katika mapinduzi ya 2023.
Ufaransa yapoteza mikataba muhimu
Hivi majuzi jeshi hilo liliondoa leseni ya kampuni ya nyuklia ya Ufaransa ya Orano ya kuchimba uranium — baada ya kuhudumu kwa miaka 50 nchini Niger. Kampuni ya Kanada GoviEX pia haina tena kibali cha kuendesha mgodi wa uranium wa Madaouela.
Makubaliano hayo mapya yanakamilisha uchimbaji wa rasilimali za madini, ambayo yanapatikana kwa wingi katika mataifa ya Sahel ya Mali, Niger na Burkina Faso.
Niger, kwa mfano, ina amana kubwa ya uranium, bati na fosfeti, pamoja na mafuta yasiyosafishwa. Burkina Faso ina shaba, zinki na manganese. Mali ina maeneo kadhaa ya mafuta ambayo hayajatumika hapo awali. Nchi zote tatu zina amana kubwa za dhahabu.
Soma pia:Niger, Burkina Faso na Mali zaombwa kurejea ECOWAS
Seidik Abba, mkuu wa taasisi ya washauri wa Sahel CIRES, yenye makao yake mjini Paris anasema "kwa muda mrefu kumekuwa na hamu kubwa ya mseto katika mahusiano ya kimataifa katika nchi hizi."
Abba ameeleza katika mahojiano na DW kwamba hata baada ya mwisho wa enzi ya ukoloni, mahusiano ya kiuchumi na nchi za Magharibi hayakuwa yenye usawa.
Nchi zote tatu pia zinafuata mkondo dhidi ya mataifa ya Magharibi na zinatafuta washirika wapya: Urusi inataka kufaidika na uchimbaji wa uranium kupitia kampuni yake ya nyuklia ya Rosatom; nayo kampuni ya uchimbaji madini ya Azelik inamilikiwa na China pakubwa.