Wataalamu wakutana Dar es Salaam kujadili kilimo na lishe
24 Juni 2025Wamejadili changamoto na fursa za mabadiliko ya tabia nchi katika sekta ya chakula na lishe, pamoja na mbinu za kuimarisha mifumo endelevu, salama na rafiki kwa mazingira.
Mkutano huo, ulioandaliwa na Shule ya Afya ya Uingereza kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), umekutanisha wadau wa kilimo na lishe kutoka nchi mbalimbali, ukilenga changamoto za mabadiliko ya tabia nchi katika mifumo ya chakula na lishe.
Profesa Sunnetha Kadilaya kutoka Chuo Kikuu cha Afya cha Uingereza amesema mkutano huu unatoa jukwaa muhimu kwa wataalamu wa sekta mbalimbali kushirikiana katika kutafuta suluhu jumuishi dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kwenye kilimo na afya ya jamii.
"Wiki ya ANH hapa Tanzania ni mfano halisi wa mshikamano wa kimataifa na uongozi wa kikanda katika kuendeleza mifumo ya chakula iliyo endelevu na jumuishi, kwa lengo la kuboresha afya na lishe kwa wote,” alisema Prof. Kadilaya.
Mkutano huu utafanyika wakati ambapo dunia inapitia changamoto za mabadiliko ya tabia nchi yanayohatarisha usalama wa chakula na lishe.
WFP: Zaidi ya watu mil 295 walikumbwa na njaa kali
Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), zaidi ya watu milioni 295 katika nchi 53 walikumbwa na njaa kali mwaka 2024 — ongezeko la takriban milioni 14 kutoka mwaka uliotangulia.
Afrika Mashariki iliathirika zaidi, huku mafuriko yakiharibu mashamba, mifugo na usambazaji wa chakula. Tanzania ilikumbwa na mafuriko kati ya Aprili na Mei 2024, yakisababisha kupungua kwa uzalishaji wa chakula kwa asilimia 30 na kuongeza uhaba, hasa vijijini.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), watu zaidi ya milioni 295 katika nchi 53 walikumbwa na njaa kali mwaka 2024 — ongezeko la takribani watu milioni 14 ikilinganishwa na mwaka uliopita.