Wataalamu wa UN wahimiza uchunguzi wa mauaji ya halaiki Mali
30 Aprili 2025Kundi la wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa limeeleza kusikitishwa kwao baada ya kugunduliwa kwa miili kadhaa karibu na kambi ya jeshi la Mali wiki iliyopita, siku chache baada ya jeshi na mamluki wa Urusi kuwakamata raia kadhaa.
Kupitia taarifa, wataalamu hao wameihimiza mamlaka nchini Mali kufanya uchunguzi wa haraka, wa kina na usio na upendeleo juu ya mauaji hayo na kutoweka kwa watu kwa kulazimishwa.
Soma pia: Ukraine yakanusha kusambaza droni kwa waasi nchini Mali
Mali, iliyoko chini ya utawala wa kijeshi kufuatia mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021, imekuwa ikikabiliwa na hali ya ukosefu wa usalama kwa zaidi ya muongo mmoja, hali inayochochewa zaidi na wapiganaji wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda na kundi linalojiita Dola la Kiislamu.
Utawala huo wa kijeshi umevunja ushirikiano wao wa muda mrefu na iliyokuwa koloni lake la zamani, Ufaransa na badala yake kushirikiana na Urusi.