Wasiwasi wazidi kuongezeka katika mji wa Uvira, DRC
4 Septemba 2025Mashuhuda wanasema kwa siku tatu mfululizo hakuna shughuli zozote zinazofanyika. Masoko, maduka, ofisi zimefungwa, na hata usafiri wa barabarani hakuna. Asasi za kiraia zimeshirikiana na kundi la wapiganaji wanaoitwa Wazalendo kudai naibu kamanda huyo wa jeshi la FARDC Olivier Gasita aliyepelekwa huko na mamlaka yakijeshi aondoke.
Ujumbe uliosambazwa na Wazalendo kwenye mitandao yakijamii tangu siku ya jumatatu umemkosoa kamanda huyo kutokana na kabila lake la Banyamulenge, anatuhumiwa kuchangia kuanguka kwa Bukavu katika mikono ya AFC/M23 mnamo mwezi Februari. Alphone Mufariji ni mwenyekiti wa harakati dhidi ya maadili mabaya, kwa kifupi MCLA mjini Uvira, anabaini kwamba madai hayo ni kwa nia ya usalama wa mji wa Uvira.
Mapigano yashuhudiwa mjini Uvira
Milio ya risasi imesikika tangu usiku katika kata mbalimbali za mji wa Uvira, vijana wenye hasira pia wamefunga njia nakuwasha moto kwenye barabara ya Kavinvira inayopelekea Burundi.
Jean-Chrisostome Kijana ni mwanaharakati wa jukwaa linaloitwa Pamoja kwa amani, anahofia kwamba madai yasasa ya wakazi wa Uvirayanaweza kuwa na madhara kiusalama na anawaonya kuepuka chuki kwa misingi ya kikabila.
Katika taarifa yahivi karibuni, Naibu Meya wa Uvira Kifara Kapenda Kiky ametoa wito kwa waandamanaji kuwajibika na kuwa na heshima kwa taasisi za Kongo na Rais wake. Pia Ameahidi kukutana nao siku ya Ijumaa kwa majadiliano zaidi. Jeshi la Kongo pia lilionya wakazi wa Uvira kutulia na kulitegemea.