Wasiwasi watanda mapigano yakiibuka kati ya M23 na Wazalendo
18 Agosti 2025Mapigano ya hivi karibuni yametokea Jumanne kati ya kundi la AFC/M23 na Wazalendo katika vijiji vya Kizuka na Muhuzi wilayani Mwenga, hadi vijiji vya Muhemba na Tubemba vinavyopakana na wilaya ya Uvira.
Mapigano kati ya AFC/M23 na wazalendo yalitokea katika kijiji cha Kaliki katika eneo la Waloayungu. Milio ya silaha nzito ilisikika hadi Kibati. Mapigano haya yaliwafanya wakaazi wa Kaliki, pamoja na watu wengine kukimbia makazi yao.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa AFC/M23 walipewa Rasimu ya makubaliano ya amani jana jumapili, kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani siku chache zijazo. Habari hii imetangazwa na afisa wa Qatar nchi mojawapo inayoratibu mazungumzo hayo.
Afisa huyo amesema Qatar kwa sasa inaandaa kikao kikubwa huko Doha, kinacholenga kufuatilia utekelezaji wa Tamko la Kanuni lililosainiwa mwezi Julai kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na M23, ili kukamilisha makubaliano ya amani. Qatar imesisitiza kuendelea katika mawasiliano na washirika wake wanaoaminika, hasa Umoja wa Afrika na Marekani.
Qatar yahakikisha mazungumzo ya amani yataendelea
Majadiliano ya moja kwa moja yaliyopangwa kufanyika tarehe 8 Agosti huko Doha kati ya serikali ya Kongo na waasi wa AFC/M23 hayakufanyika, wala wajumbe wa pande hizo mbili hawakufika. Licha ya kizuizi hiki cha wazi, upatanishi wa Qatar umehakikisha kuwa pande hizo mbili zinaendelea na majadiliano ndani ya mfumo wa utekelezaji wa Azimio la Kanuni.
Moja ya mambo muhimu yaliyojadiliwa ni kuruhusiwa kwa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na utaratibu wa kubadilishana wafungwa, mchakato ambao huenda ukachukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa, ingawa mpatanishi amehakikisha kwamba unaendelea.
Tamko la Kanuni, lililotiwa saini mjini Doha, lililazimisha pande zote mbili kuhakikisha kunapatikana amani ikiwa ni pamoja na kuachiliwa kwa wafungwa kutoka pande zote mbili hadi ifikapo Julai 29 kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya moja kwa moja Agosti 8. AFC/M23 imetishia kutorejea kwenye mazungumzo hayo mjini Doha kabla ya kuachiliwa kwa wapiganaji wake wapatao 700 waliozuiliwa.
AFC/M23 wailaumu serikali kwa kukwamisha mazungumzo ya Doha
Akiongea na wanahabari mjini Bukavu mwishoni mwa juma, gavana wa Kivu Kusini chini ya AFC/M23 Patrick Busu bwa Ngwi ametangaza kwamba hivi karibuni atataja serikali yake mpya na kuiwamgia lawama Kinshasa kwa kukwamisha mazungumzo ya Doha.
"Kwa sasa mazungumzo yamesimama kwa sababu hatua za kujenga imani tulizoomba kutoka kwa serikali ya Kinshasa hazijazingatiwa. Naamini wakuu wetu wanajisughulisha na hili. Sisi tumejitolea kuwa na amani. Lakini tuko tayari na mara tu watakapotushambulia tutajibu."
Haya yakijiri, jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeahidi kulivalia njuga suala la usalama katika eneo la mashariki mwa Kongo na kulinda wakazi wa miji ya Beni na Lubero dhiri ya mashambulizi ya waasi wa ADF. Jumapili, watu tisa walipoteza maisha katika shambulizi lilanotajwa kufanywa na ADF katika eneo la Oicha, katika jimbo la Kivu ya kaskazini.