Wasiwasi waongezeka kuhusu vita vya Iran na Israel
23 Juni 2025Mzozo kati ya Iran na Israel unazidi kutanuka, baada ya Marekani kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Iran mwishoni mwa juma. Hivi leo, kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amemtuma waziri wake wa mambo ya nje mjini Moscow kuomba usaidizi kwa Rais Vladmir Putin.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Aragchi amekwenda Moscow kuomba usadizi wa Urusi baada ya Marekani kufanya mashambulio makubwa ya kijeshi dhidi ya maeneo ya shughuli za nyuklia ya Iran, mashambulio hayo yakiwa ya kwanza kufanywa na Marekani tangu mapinduzi ya Jamhuri hiyo ya kiislamu mwaka 1979.
Hivi leo Israel nayo imesema inaendelea kushambulia katika mji wa magharibi wa Iran wa Kermanshah huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu kutanuka kwa vita hivyo na kuwa vya kikanda.
Rais wa Marekani Donald Trump sio tu ameionya Iran dhidi ya kufanya mashambulio ya ulipaji kisasi, bali amezungumzia pia juu ya uwezekano wa kufanyika mabadiliko ya kiutawala ndani ya Iran.
Yote hayo yameongeza wasiwasi duniani kuhusu hatma ya mzozo huu huku bei ya mafuta ikipanda zaidi ya asilimia 4 leo Jumatatu.
Wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa
Viongozi wa ulimwengu wanaonesha kuwa na wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kutanuka vita hivi,ambapo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, katika mkutano wa dharura wa bazara la usalama, uliotishwa jana alionya dhidi ya kuendelea kwa mashambulio ya kulipiziana kisasi wakati China nayo hivi leo ikitahadharisha dhidi ya kusambaa kwa vita hivyo huku ikiitolea mwito jumuiya ya kimataifa kuchukuwa hatua zaidi kuzuia vita hivyo kuathiri uchumi wa dunia.
China imezungumzia umuhimu wa njia ya bahari ya Ghuba katika pwani ya Iran. Viongozi wa Uingereza Ufaransa na Ujerumani wameitaka Iran kutochukua hatua zaidi ambazo zinaweza kuathiri uthabiti wa kanda hiyo.
Katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya, mjini Brussels mawaziri wa mambo ya nje wamekusanyika na suala la Iran na Israel ndiyo ajenda kubwa kwenye kikao hicho.
Mkuu wa sera za nje na masuala ya usalama Kaja Kallas ambaye pia ni makamu wa rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, amesema Umoja huo unawasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi ya kulipiziana kisasi na kutanuka kwa vita hivi.
''Leo tutakuwa na mkutano mrefu wa baraza la mambo ya nje,Tumeshaijadili Iran lakini bila shaka tutajadili zaidi suala hilo.Mawaziri wanajikita zaidi katika kutafuta suluhisho la kidiplomasia na pia kutazama wasiwasi mkubwa uliopo kuhusu mashambulizi ya kulipiziana kisasi na kutanuka vita hivi.Na hasa wasiwasi wa kufungwa na Iran kwa mlango bahari wa Hormuz,hicho ni kitu kitakachokuwa hatari zaidi na sio kizuri kwa mtu yoyote''
Wakati wasiwasi huo ukizungumziwa na viongozi wa ulimwengu,bunge la Iran tayari limeshaidhinisha hatua ya kufungwa kwa mlango bahari wa Hormuz ambao kwa hakika ndio njia muhimu kabisa ya usafirishaji mafuta duniani.
Ali Akbar Velayati, mshauri wa kiongozi wa juu zaidi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema nchi yoyote ile iliyotumiwa na Marekani kufanya mashambulizi yake dhidi ya Iran, ni halali kushambuliwa na jeshi la Iran.
Na mkuu wa shirika la kudhibiti matumizi ya nguvu za Atomiki IAEA Rafael Grossi muda mfupi uliopita amesema kwamba, Inatarajiwa kwamba uharibifu mkubwa umefanyika katika kinu cha nyuklia cha Fordo baada ya mashambulio ya Marekani yaliyofanywa kwa kutumia makombora yenye uwezo mkubwa wa kupasua miamba.
Grossi ametaka waangalizi wa shirika hilo warejee kwenye maeneo ya vinu vya Nuklia vya Iran yaliyoshambuliwa kufanya tathamini ya kina.