Sam Nujoma, rais wa kwanza wa Namibia afariki dunia
9 Februari 2025Samuel Shafiishuna Nujoma, alikuwa mpigania uhuru aliyesimama kidete mbele ya Afrika Kusini katika kupigania ukombozi wa nchi yake Namibia.
Kama kiongozi wa lililokuwa vuguvugu la kupigania uhuru lililokuja kufahamika kama chama cha SWAPO, Nujoma aliwaunganisha Wanamibia na kuifanya jumuiya ya Kimataifa kutambua mapambanao dhidi ya kukaliwa kwa mabavu na Afrika Kusini na utawala wa ubaguzi wa rangi katika Afrika Kusini.
Utawala ambao uliweka sheria kali ya kuwabagua watu kwa rangi zao na kuwanyima haki wazawa. Kujitolewa kwa Nujoma,bidii na mapenzi yake kwa Wanamibia kulileta mafanikio wakati nchi hiyo ilipopata uhuru wake mnamo mwezi March 1990, aliingoza nchi hiyo akiwa rais na kuitumikia kwa miaka 15.
Amefariki akiwa na umri wa miaka 95 Jumamosi jioni katika hospitali alikokuwa amelazwa katika mji mkuu wa Namibia, Windhoek. Alizaliwa Mei 12 mwaka 1929 kwenye eneo la Etunda Kaskazini mwa Namibia.
Alikuwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto 11 na alihusika katika kuwalea ndugu zake na kuchunga mifugo ya familia. Hakuwa na fursa kubwa ya kupata elimu lakini alipata masomo yake kwenye shule ya kimishionari na kumaliza hadi darasa la sita,ambacho ni elimu ya kiwango cha juu wakati huo kwa mtu mweusi kwenye taifa hilo.
Elimu yake na siasa zilichochewa na nini
Akiwa na umri wa miaka 17 alihamia katika mji wa Walvis Bay, ambako alifanya kazi katika duka la jumla. Na huko ndiko alikofahamu mambo mengi katika ulimwengu wa siasa baada ya kukutana na wanajeshi kutoka mataifa mbali mbali waliokuja wakati wa vita vya pili vya dunia.
Baadae Nujoma alihamia Windhoek ambako alifanya kazi kwenye shirika la reli la Afrika Kusini na huko alianza masomo ya usiku ili kuimarisha uwezo wake wa kuzungumza lugha ya kiingereza.
Philosofia yake ilikuwa ni rahisi,ilijikita zaidi katika Uhuru na utaifa, japo baadhi ya watu wanasema alikuwa zaidi na mwekeleo wa Kimaxist.
Siasa zake zilichochewa na hali ya kukosekana usawa chini ya utawala wa kibaguzi, mifumo ya ajira iliyokuwa haizingatii haki na ufahamu wake ulioongezeka kuhusu kampeini za kudai uhuru kote barani Afrika.
Mwishoni mwa miaka 1950, Nujoma alisaidia katika uasisi wa vuguvugu la kizalendo la watu wa Namibia, OvamboLand, likiwa na lengo la kuundowa utawala wa ubaguzi wa rangi lililokuja baadae kurithiwa na chama cha SWAPO.
Mwaka mmoja baade aliizunguka nchini Namibia kwa siri, akikusanya wanachama na kuiunda mifumo ya vuguvugu hilo la OPO (OvamboLand Peoples Organization) kabla ya kulazimika kukimbilia uhamishoni baada ya kuanzisha maandamano ya upinzani katika eneo la makaazi ya watu weusi lilolotengwa karibu na mji mkuu Windhoek,ambako watu walikuwa wakihamishwa kwa nguvu.
Baada ya miaka mingi ya kukosa kufanikiwa katika kuutaka Umoja wa Mataifa kuilazimisha Afrika Kusini kuipatia mamlaka yake Namibia,iliyokuwa ikijulikana kama Afrika ya Kusini Magharibi, vuguvugu la SWAPO likaanzisha mapambano ya silaha mnamo mwaka 1966.
Ingawa jeshi la wapiganaji wake ambalo likifahamika kama jeshi la ukombozi wa watu wa Namibia,PLAN, lilishindwa kukomboa eneo lolote,lilifanikiwa kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kutambua mapambano ya Wanamibia.
Mnamo mwaka 1973 Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, likaitambuwa SWAPO kama mwakilishi pekee halali wa watu wa Namibia.
Baada ya karibu miaka 30 ya kujaribu kuwakomboa Wanamibia kutoka kwa Afrika Kusini,Wanamibia wakapata uhuru wao mnamo mwaka 1990 na Sam Nujoma akarejea kutoka uhamishoni na kutwaa uongozi wa taifa hilo.Soma pia WINDHOEK : Namibia yataka utulivu baada ya Nujoma
Aliiongoza Namibia kuwa taifa la demokrasia thabiti baada ya kushuhudia karne kadhaa za utawala wa wakoloni, kukaliwa kwa mabavu pamoja na utawala wa kibaguzi.
Mafanikio aliyoyaleta Namibia
Na miongoni mwa mafanikio yake ya mwanzo kabisa ni kuweka sera ya ''maridhiano ya kitaifa'' ambayo ilikuwa na dhamira ya kuimarisha na kuleta maelewano katika mahusiano miongoni wa makabila mbali mbali ya watu wa Namibia.
Kabla ya kujiuzulu kwake kama rais, bunge la nchi hiyo lililokuwa likihodhiwa na chama cha SWAPO lilikubali kubadili katiba na kumruhusu agombee muhula wa tatu. Hatua hiyo ilivutia ukosoaji kutoka jamii ya Kimataifa na hata ndani,japo Nujoma alishinda bila upinzani mkubwa na kuingia tena madarakani mwaka 1999.
Baade alitangaza kutogombea tena kubakia madarakani kwa muhula wa nne na akajiuzulu mnamo mwaka 2005 na kumkabidhi kwa njia ya amani, madaraka mrithi wake Hikikepunye Pohamba. Nujoma alijiuzulu pia kuwa mwekiti wa SWAPO mwaka 2007.