Wasichana waliopata ujauzito kuendelea na shule Kongo
17 Julai 2025Miongoni mwa waliothamini na kupongeza tangazo hilo ni Zawadi Bagaya Bazilyene,akiwa mtetezi wa haki za wanawake kutoka kijiji cha Kavumu ndani ya jimbo la Kivu Kusini. Anaamini kuwa wasichana kadhaa wamekuwa wajawazito bila kutaka na kwamba hatua hii inawapa nafasi ya pili ya kuendelea na masomo yao kwa umakini.
"Hatua hiyo ni nzuri sana tena sana, kwasababu kuna mabinti wengi ambao wamepata mimba, kuna wanafunzi na ambao sio wanafunzi. Ni muhimu kuwahimiza viongozi wa masomo kuwarejesha shuleni kwasababu ni changamoto iliyowapata na sio kupenda kwao."
Maoni haya yanaungwa mkono na mkazi huyu wa Bukavu, Byadunia Bashimbe ambaye anakumbusha kuwa wakati wa tukio la ujauzito kati ya vijana ni hasa msichana mwanafunzi ambaye ni anapoteza zaidi kuliko mvulana.
"Wakati atakapobeba mimba kijana wa kiume yeye anaendelea na shule ila yule wa kike anbaki nyumbani. Msichana anatakiwa kusoma atakapojifungua. Maana atakuwa na haja ya elimu na ajira."
Uamuzi huenda ukachangia kupotea kwa maadili kwa mtoto wa kike
Amina pia ni mkazi wa Bukavu ambaye anajiuliza ikiwa walimu wako tayari kuvumilia changamoto za mimba za wanafunzi. Amesema mimba inakuwa na changamoto nyingi na kuhoji iwapo wasichana wanaweza kustahamili changamoto hiyo wakiwa darani.
Akiwa kiongozi wa shirika la wazazi wa wanafunzi wa Kongo, kwa kifupi ANAPECO/Kivu Kusini, Mulumeonderhwa Batandi Augustin anatupilia mbali uamuzi huo wa Waziri wa Elimu ya Kitaifa, na anamtaka ayape kipaumbele mambo mengine muhimu kuboresha elimu akisema hatua hiyo huenda ikasababisha upotevu wa wasichana wakike na kukuza tabia mbaya miongoni mwa jamii.
Katika taarifa iliyotiwa saini Julai 14, Waziri wa Elimu ya Kitaifa na Uraia Mpya Nchini Kongo, Raissa Malu alionyesha kuwa uamuzi huu ambao utaanza kutumika kuanzia mwaka ujao wa shule mwezi Septemba unalenga kuwahakikishia wasichana kufikia mfumo wa elimu jumuishi na usawa wa kijinsia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.