Washirika wa Ukraine waahidi msaada wa euro bilioni 21
11 Aprili 2025Waziri wa ulinzi wa Uingereza, John Healey, leo ametangaza kwamba washirika wa Ukraine wa jumuiya ya kujihami NATO wameahidi kutoa msaada wa kijeshi wa thamani ya zaidi ya euro bilioni 21 huku nchi hiyo ikiendelea kushambuliwa na Urusi. Healey amesema mwaka huu ni muhimu katika vita vya Ukraine.
Healey alikuwa akizungumza katika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa kwa pamoja na mawaziri wa ulinzi wa Uingereza na Ujerumani kuratibu msaada zaidi wa kijeshi kwa ajili ya Ukraine katika makao makuu ya jumuiya ya NATO mjini Brussels.
Kaimu waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema msaada huo utakuwa na mchango muhimu katika uwanja wa mapambano mwaka huu akitambua kuwa amani nchini Ukraine inaonekana kuwa mtihani kuifikia katika kipindi kifupi kijacho.