Washirika ´kuimwagia´ Ukraine zana zaidi za kijeshi
15 Julai 2025Waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani amekutana na mwenzake wa Marekani Pete Hegseth usiku wa kuamkia leo na kutangaza kuwa mifumo miwili ya ulinzi wa anga chapa Patriot inaandaliwaa kwa ajili ya kupelekwa Ukraine.
Waziri Pistorius amesema ununuzi huo utafadhiliwa na Ujerumani na mipango ya jinsi ya kuifikisha mifumo hiyo nchini Ukraine inaandaliwa.
Ziara ya Pistorius imefanyika wakati utawala wa Rais Donald Trump umebadili mkondo na sasa unafanya kazi kwa karibu zaidi na washirika wake wa Ulaya kuisaidia Ukraine kukabiliana na Urusi.
Trump ambaye aliingia madarakani akitoa ahadi ya kuvimaliza vita vya Ukraine ndani ya muda mfupi, amesema amefadhaishwa na tabia isiyotabirika ya Rais Vlamidir Putin wa Urusi, aliyemtaja wakati wa kampeni zake za uchaguzi mwaka uliopita kuwa "kiongozi wanayeheshimiana."
Hapo jana Trump alitishia kuwa anapanga kuchukua hatua kali za kiuchumi dhidi ya Urusi kutokana na dhima yake kwenye vita vya Ukraine.
Kwenye tangazo lake lililosubiriwa kwa shauku Trump amesema atailenga Urusi kwa kuyawekea ushuru wa hadi asilimia 100 mataifa yote yanayofanya biashara na Moscow.
Uamuzi huo utashuhudia nchi yoyote iliyo na mafungamano ya kibiashara na Urusi ikilipa gharama hizo pale inapotaka kuuza bidhaa zake nchini Marekani. Amesema hatua hizo zitachukuliwa iwapo mkataba wa amani hautapatikana ndani ya muda wa siku 50.
Wachambuzi wanasema ikiwa Trump atatekeleza mpango huo, Urusi huenda itapoteza washirika wachache wa kibiashara waliosalia na uchumi wake utetereka na hivyo kupunguza nguvu ya kifedha ya kuendelea kufadhili vita nchini Ukraine.
Ahadi ya silaha yadhihirisha mabadiliko ya mtazamo mjini Washington
Mbali ya kitisho cha hatua za kiushuru, Trump pia ametangaza kwamba Marekani itaipatia silaha za kisasa zaidi Ukraine ili ikabiliane na Urusi.
Ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami NATO, Mark Rutte aliye ziarani nchini Marekani.
Mpango huo utahusisha mauzo ya silaha za Marekani zenye thamani ya mabilioni ya dola kwa nchi za Ulaya ambazo zenyewe zitaipatia Ukraine.
Rutte amesema Ujerumani, Canada, Norway, Sweden, Uingereza na Denmark ni miongoni mwa nchi zilizo tayari kununua silaha za Marekani na kuzipeleka nchini Ukraine. Mnamo siku ya Jumapili, Trump alitoa idhini ya kutumwa mifumo ya ulinzi wa anga aina ya Patriot kwa Ukraine.
Mifumo hiyo imekuwa ikiombwa kwa muda mrefu na utawala mjini Kyiv unaosema ni muhimu kuisaidia Ukraine kujilinda na mashambulizi yanayozidi makali kutoka Urusi. Mifumo ya Patriot hutoa ulinzi kwa kudungua makombora ya masafa na hata ndege za kivita za adui.
Zelenskyy amshukuru Trump kwa "utayari wake wa kuisaidia Ukraine"
Utawala wa Trump ulikuwa unasuasua kuendelea kutuma silaha nchini Ukraine ukiamini kuwa mkakati huo ungemshawishi Putin kuvimaliza vita na kufikiwa mkataba wa amani.
Hata hivyo hilo halijafanikiwa na badala yake Moscow imeendelea kuvurumisha makombora na droni huku mazungumzo ya amani ni kama yamesambaratika.
Katika hatua nyingine, Rais Volodymyr Zelenskyy amefanya mazungumzo na Trump hapo jana jioni baada ya kutolewa tangazo kuwa nchi yake itapatiwa silaha zaidi kutoka Washington kupitia kwa washirika wa Ulaya.
Zelenskyy amesema mazungumzo yao yalikuwa mazuri na alimshukuru Trump kwa kile amekitaja kuwa "utayari wake wa kuisaidia Ukraine na kufanya kazi pamoja kuvimaliza kupitia vita kwa njia ya haki."