WASHINGTON:Majeshi yaMarekani yadai hakuna uharaka kuwamaliza wanamgambo nchini Iraq.
28 Septemba 2005Taarifa iliyotolewa na jeshi la Marekani imeeleza kuwa hakuna uharaka unaooneshwa wa kuwamaliza wanamgambo wa Iraq,licha ya kuuawa kwa kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa kundi la al-Qaeda nchini humo juzi siku ya Jumatatu.
Mkuu wa majeshi ya Marekani,Jenerali Richard Myres,amesema kuuawa kwa Abu Azzam kunaweza kuwa na mguso fulani,lakini hata hivyo nafasi yake itajazwa haraka.
Msemaji wa majeshi ya Marekani amedai kuwa Abu Azzam alikuwa mtu wa karibu sana wa Abu Musab al-Zarqawi,kiongozi wa kikundi cha al-Qaeda nchini Iraq,ambaye hadi sasa majeshi ya Marekani yanamtafuta kwa udi na uvumba.
Taarifa zaidi iliyotolewa na jeshi la Marekani imeeleza Abu Azzama lipigwa risasi na majeshi ya Iraq yaliyokuwa yakiongozana na ya Marekani kumsaka mtu huyo baada ya kuwepo taarifa za kipelelezi za mahala alipokuwa amejificha.
Katika taarifa nyingine usiyokuwa na uthibitisho kupitia mtandao wa internet,kikundi cha al-Qaeda,kimekanusha madai kuwa Abu Azzam alikuwa ni mtu pili kwa Zarqawi.
Wakati huo huo,jeshi la polisi nchini Iraq limesema wamegundua miili 22 ya wanaume ambao walikuwa wamefunikwa macho na kupigwa risasi karibu na mpaka wa mji wa Kut.