WASHINGTON: Rumsfeld amesema maafisa wa Marekani wamekutana na waasi nchini Iraq
27 Juni 2005
Maafisa wa Kimarekani nchini Iraq wamewahi kufanya majadiliano pamoja na viongozi wa waasi.Hiyo ni kwa mujibu wa waziri wa ulinzi wa Marekani,Donald Rumsfeld.Katika mahojiano yake na stesheni ya televisheni ya Fox News,Rumsfeld alisema mikutano ya aina hiyo ilifanywa mara kwa mara na kwamba suala hilo linakuzwa kupindukia kiasi.Waziri Rumsfeld alieleza hayo,baada ya gazeti la Uingereza,“Sunday Times“ kuripoti kuwa mikutano miwili ya aina hiyo ilifanywa kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq,Baghdad.Ripoti hiyo imesema, makamanda wa waasi walikutana na maafisa wanne wa Kimarekani uso kwa uso,wakati wa majadiliano yao mapema mwezi huu wa Juni.Walioshiriki katika mikutano hiyo ni wajumbe wa kundi la Ansar al Sunna“ lililofanya idadi fulani ya mashambulio ya kujitolea muhanga maisha na pia wa makundi mengine yasiojulikana sana.Kundi la Ansar lakini limekanusha kukutana na maafisa wa Kimarekani.