WASHINGTON : Repoti ya siri juu ya Iraq yatangazwa
27 Septemba 2006Kwa mujibu wa baadhi ya vipegele vya repoti ya siri ya usalama kuhusu Iraq ambayo imetangazwa na utawala wa Rais George W Bush wa Marekani hapo jana vita vya Marekani nchini Iraq vinachochea kizazi kipya cha viongozi wa magaidi.
Bush alisema alikuwa hakubaliani na hitimisho lililotolewa na baadhi ya watu kwa kufungamanisha vita nchini Iraq na ugaidi. Rais huyo wa Marekani alikasirishwa kwa namna repoti hiyo ya siri iliokamilishwa hapo mwezi wa April na baadhi ya vipengele vyake kuchapishwa hivi karibuni na gazeti la New York Times ilivyochukuliwa vibaya na kuamuru itangazwe.
Repoti hiyo inasema makundi ya kigaidi yaliotawanyika yanazidi kutapakaa na kujiweka katika hali nzuri ya kupambana na hatua za kupiga vita ugaidi jambo ambalo linafanya iwe vigumu kuwapata magaidi hao na kuwadhoofisha.
Baadhi ya vipengele vya repoti hiyo ambavyo vimetangazwa hapo jana vimetaja mambo manne makuu yanayosababisha ugaidi kuzagaa ambayo ni manun’guniko ya muda mrefu yalioko katika ulimwengu wa Kiislam,vita takatifu vya Jihad nchini Iraq, kuzorota kwa mwendo wa mageuzi katika nchi nyingi za Kiislam na chuki dhidi ya Marekani.