WASHINGTON Marekani na Uingereza kutafuta njia za kufuta madeni ya Afrika
8 Juni 2005Rais George Bush wa Marekani na waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair wamesema kuwa nchi zao zinatayarisha mpango juu ya kuzifutia madeni yote nchi za Afrika.
Viongozi hao waliyasema hayo walipofanya mkutano na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao kwenye ikulu ya White House mjini Washington.
Hata hivyo viongozi hao pia wamezitaka nchi za Afrika zijizatiti katika kutekeleza uongozi bora, kuikabili rushwa na kurekebisha uchumi wao.
Akisisitiza dhamira ya kuzisaidia nchi za Afrika waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair amesema pamoja na kufuta madeni yote ya Afrika, nchi tajiri zinapaswa pia kuongeza misaada.
Bwana Tony Blair yupo Marekani katika kutayarisha mkutano wa nchi 8 tajiri duniani utakaofanyika mwezi ujao nchini Scotland ambapo Uingereza itakuwa mwenyekiti.
Bwana Blair ambaye pia ni mwenyekiti wa tume ya kuondoa umasikini barani Afrika atalipa kipaumbele swala la Afrika katika ajenda ya mkutano huo.
Nchi za Afrika zinazodaiwa kiasi cha dola bilioni 80 zinalipa takriban hadi dola bilioni 13 kila mwaka kama riba.
Hata hivyo wadadisi wanasema kwamba kufutwa kwa madeni na kuongezwa kwa misaada pekee kwa bara la Afrika, hakutasaidia bila ya nchi tajiri kuweka wazi masoko yao kwa bidhaa za kutoka Afrika.
Wakati huo huo Marekani imeahidi msaada wa dola milioni 674 kwa ajili ya kupambana na baa la njaa katika nchi za upembe wa Afrika.