Washington: Marekani imetangaza itapeleka wanajeshi zaidi nchini Iraq.
27 Novemba 2003Matangazo
Waziri wa ulinzi wa Marekani, Donald Rumsfeld, amekubali watumwe wanajeshi wengine 3,000 wa nchi kavu. Uamuzi huu ni sehemu ya matayarisho juu ya mpango wa kuwabadilisha wanajeshi walioko huko hivi sasa. Pia Shirika la habari la Kitaliana limesema roketi moja lililipiga jana jengo la ubalozi wa Italy ulioko Baghdad. Jengo hilo liliharibika lakini hamna mtu aliyeumia. Mwanzoni mwa mwezi huu, shambulio la kujitolea mhanga liliwauwa wanajeshi 19 wa Kitaliana katika mji wa kusini wa Nassiriya. Tangu wakati huo majeshi ya Italy katika Iraq yamewekwa katika hali ya tahadhari. Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Uengereza, Jack Straw, akimaliza ziara yake ya siku mbili nchini Iraq, alikuwa jana na mkutano na waandishi wa habari mjini Baghdad, huku akilindwa vikali. Alikiri kwamba Muungano unaoongozwa na Marekani bado haujaweza kuushinda upinzani wa kisilaha katika nchi hiyo, lakini alielezea matumaini kwamba hali itaendelea kutulia. Bwana Straw alisema mashambulio yanayoendelea kufanywa dhidi ya majeshi ya Muungano sio jambo lilozistaajabisha serekali za Uengereza na Marekani.